Sakata la watumishi wa umma kushughi vyeti vya elimu limezidi kuchukua sura mpya na sasa wamefikia zaidi ya 10,000.
Hatua hiyo, inatokana na uhakiki uliofanywa na Sekretarieti ya Ajira
katika Utumishi wa Umma ambayo imebaini waombaji kazi 39,511 kati yao,
1,951 wana vyeti vya kughushi.
Kuongezeka kwa idadi hiyo, kunatokana na kauli ya Rais Dk. John
Magufuli, wiki iliyopita, kwamba anasubiri ripoti ya wafanyakazi wa
Serikali ambao wamebainika kuwa na vyeti feki.
Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam, wakati akizindua mabweni mapya ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Alisema anafahamu idadi ya watumishi wenye vyeti feki ni zaidi ya 9,000 na anaisubiri ripoti hiyo kuifanyia kazi.
“Kwa hiyo mnaweza mkaona shida zilizopo katika nchi hii, huku
wafanyakazi hewa karibu 19,000, wanafunzi hewa ni zaidi ya 56,000, kila
mahali unapokwenda ni matatizo, lakini ni lazima niyatatue matatizo kwa
sababu mlinichagua kwa ajili hiyo,” alisema Rais Magufuli.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 kwa ofisi yake jana
bungeni mjini hapa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema baada ya
kubainika kwa hali hiyo, wahusika waliondolewa kwenye mchakato, huku
vyeti hivyo vikiwasilishwa katika mamlaka husika kwa hatua za kisheria.
“Wahusika waliondolewa katika mchakato pamoja na vyeti hivyo kuchukuliwa
na kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema
Kairuki.
Hata hivyo, zipo taarifa zinazodai kuwa orodha ya watumishi wa umma
ambao wamebainika kuwa na vyeti feki itawekwa hadharani Aprili 30.
Zaidi inaelezwa kuwa sakata hilo la vyeti feki linawagusa pia mabalozi
ambao ni wawakilishi wa Watanzania katika mataifa mbalimbali, wakuu wa
wilaya na mikoa.
Tags
Vyeti Feki
