WAFANYAKAZI 16 wa kampuni ya Quality Group Ltd, wamehukumiwa kulipa
faini ya Sh. 500,000 au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukiri makosa
ya kufanya kazi nchini bila kibali. Jumla ya faini yote ni Sh. milioni
22.
Hukumu hiyo ilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar
es Salaam, baada ya washtakiwa kukiri mashtaka yanayowakabili. Quality
Group Ltd ni kampuni ya mfanyabiashara Yusuph Manji.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi Cyprian Mkeha, alisema
mshtakiwa wa kwanza hadi 14 wanakabiliwa na mashtaka matatu hivyo katika
kila kosa kila mmoja atatoa faini ya Sh. milioni 1.5.
Pia alisema kama watashindwa kulipa faini hiyo, kila mshtakiwa
atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela katika kila kosa, hivyo
watatumikia kifungo cha miaka tisa jela.
Kwa upande wa washtakiwa namba 15 na 16, Meneja mradi Jose Kiran na
katibu wake, Prakash Bhatt, wanaokabiliwa na tuhuma za kukiuka amri ya
ofisa uhamiaji na kujaribu kutoroka, wamehukumiwa kulipa faini ya Sh.
500,000 au kwenda jela miaka mitatu. Wamekwepa kifungo kwa kulipa faini.
Jose na Prakash wanadaiwa kuwa Februari 20, 2017, wakiwa raia wa India
na waajiriwa wa Quality Group Ltd, walimzuia ofisa wa Uhamiaji kufanya
kazi zake na kwamba walikataa kuripoti katika ofisi za Uhamiaji zilizoko
jijini Dar es Salaam kwa kujaribu kutoroka Tanzania kupitia mpaka wa
Horohoro, Tanga.
Washtakiwa 14 waliobaki ni mshauri Jagadish Mamidu (29), mshauri Niladri
Maiti (41), mshauri Divakar Rajasekaran (37), Mhasibu Mohammad Taher
Shaikh(44), mshauri Bijenda Kumar (43) na mshauri Prasoon Kumar
Mallik(46).
Wengine ni mshauri Nipun Dinbadhu Bhatt (32), Meneja Msaidizi Pintu
Kumar (28), mshauri Anuj Agarwal (46), mshauri Varun Boloor (34),
mshauri Arun Kumar
Kateel (46), mshauri Avinash Chandratiwari (33) na mshauri Vikram Sankhala (50). Nao walilipa faini na kukwepa vifungo hivyo.
Mahakama imesema ili waweze kuendelea kuishi nchini ni lazima wafuate sheria.
Wakili wa washtakiwa hao, Hudson Ndusyepo kabla ya hukumu kutolewa
aliiambia mahakama mshtakiwa namba moja hadi 14 hawakuwa na nia mbaya ya
kutenda makosa hayo.
Alidai kuwa walikutana na Afisa wa Uhamiaji wakamwambia wanahitaji
kuongeza muda wa viza za kufanya kazi na wakamkabidhi hati zao za
kusafiria na baadae aliwarejeshea zikiwa na visa ndani.
Aliendelea kudai kuwa wao waliamini viza hizo zilipatikana kwa halali na
malipo yalifanyika na fedha kuingia Serikalini kupitia mpaka wa
Tunduma, na kwamba risiti walipata.
Aliendelea kudai kuwa baada ya kukamatwa iligundulika viza hizo zilipatikana kinyume cha sheria.
Alieleza hilo ni kosa lao la kwanza na akaomba mahakama iwasamehe,
wapewe adhabu ndogo na nafasi nyingine ya kuwepo nchini na kwamba
watafuata taratibu za nchi hii.
Kwa upande wa Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma
yeye alidai kuwa washtakiwa hao waliingia nchini mwishoni mwa mwaka jana
na wakapewa viza za miezi mitatu za kufanya kazi.
Alidai kuwa baada ya vibali hivyo kwisha walifanya wanavyojua, ikiwamo kutoa maelezo ya uongo na kufanikiwa kujipatia viza hizo.
Kwa pamoja walidaiwa kuwa Februari 13 katika Kampuni ya Quality Group
Ltd iliyopo wilaya ya Ilala, wakiwa raia wa India walikamatwa wakiwa na
viza za kibiashara zilizoghushiwa.
Wanadaiwa kuwa Februari 13 katika kampuni hiyo ya Quality Group Ltd
washtakiwa hao wakiwa raia wa India walikamatwa wakiishi nchini kinyume
cha sheria.
Iliendelea kudaiwa kuwa Februari 13 washtakiwa hao wakiwa raia wa India
walikamatwa wakifanya kazi katika kampuni ya Quality Group Ltd kama
washauri bila ya kuwa na kibali kinachowaruhusu kufanya hivyo.
Washtakiwa waliachiwa baada ya kulipa faini zao.
