Muimbaji wa nyimbo za injili madam Flora (Zamani Flora Mbasha) amekiri
kupata mtoto nje ya ndoa yake na aliyekuwa mume wake Emmanuel Mbasha
ambaye pia ni muimbaji wa nyimbo za injili. Imefahamika.
Hilo limefichuliwa leo na aliyekuwa mumewe, Emmanuel Mbasha, alipokuwa
kwenye kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa kupitia ukurasa wa facebook
wa EATV kila siku ya Jumatano kuanzia saa nane kamili mpaka saa kumi
jioni.
Ishu hiyo imeibuka baada ya mmoja kati ya watu waliouliza maswali,
kumtaka Mbasha kunyoosha maelezo kuhusu mtoto wa pili wa Flora kama ni
wake ama la, na ndipo Mbasha akaweka wazi kuwa mtoto yule si wake, na
Flora mwenyewe alishakiri suala hilo.
Mbasha amesema kuwa, Flora alikiri suala hilo hivi karibuni wakiwa
katika harakati za kuachana kwa mujibu wa sheria mahakamani, ambapo
ilipofika wakati wa kutaja idadi ya watoto aliozaa naye, Flora alimtaja
mtoto mmoja pekee ambaye ni Elizabeth (akiwa ni mtoto wao wa kwanza)
"Yule mtoto siyo wangu, hata katika hati ya mashitaka ya kuachanishwa na
mahakama, yeye mwenyewe Flora kwa mkono wake akiwa na wanasheria wake,
aliandika kwamba kwa kipindi chote ambacho aliishi na mimi alibahatika
kupata mtoto mmoja pekee ambaye ni Eliza, kwahiyo mpaka hapo unajua
kabisa kwa hapa imeshakula kwangu, ni kitu ambacho kinauma sana, lakini
kila mtu na ujasiri wake" Alisema Mbasha.
Kuhusu uamuzi aliouchukua baada ya kuthibitishiwa hilo, Mbasha amesema
"Nilipojua siyo wa kwangu nilikaza moyo, nikasema basi Mungu ana
makusudio yake, lakini kama ningeichukulia kibinadamu, ningeushangaza
ulimwengu na dunia"
Kuhusu uwezekano wa kurudiana na Flora, Mbasha amesema kuwa yeye na
Flora mapenzi yao yalishakwisha kutokana na mwenza wake huyo kuamua
kuanza maisha mapya na kumuacha yeye.
Wakati akijibu moja ya swali kutoka kwa shabiki aliyetaka kujua ni jambo
gani lililopelekea yeye kuachana na mkewe Flora Mbasha ndipo hapo
Mbasha alifunguka na kusema yeye hajamuacha
mkewe, bali mkewe ndiye alimuacha yeye kwa kumsaliti na mtu mwingine kwa
sababu za kimaslahi na tamaa kutokana na umaarufu uliowafanya waweze
kuonana na watu wengi wenye uwezo wa kila aina kifedha ikiwemo viongozi
wa serikali na wafanyabiashara.
"Mimi siwezi kusema nilimuacha mke wangu, bali mwenzangu tayari alikuwa
na maisha mengine yaani tayari alikuwa na njia zake na alishakuwa
amefanya maamuzi na kuamua kwenda na njia ambayo yeye aliona ni sahihi
na kuendelea na maisha yake. Hivyo alinisaliti kwa sababu ya maslahi na
kwenda kwingine ambako anaona ni sehemu sahihi kwake" alisema Mbasha
Msanii huyo anakiri kuwa kitendo hicho kilimuumiza sana na kumtesa
lakini yeye alimtumaini na kumuomba Mungu kwani hakutaka kuvuta bangi,
au kunywa pombe ili kuondokana na 'stress' bali alimuomba Mungu na Mungu
alimsaidia kupita katika kipindi hicho kigumu.
Kuhusu kuoa tena, Mbasha amesema hana mpango wa kuoa kwa kuwa hajapata mtu wa kuoa, hivyo ameamua kubaki 'single boy'
Katika hatua nyingine amesema hawezi tena kwenda wala kuhudhuria ibada
katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat
Gwajima baada ya kukosana na mtu mmoja ambaye hajamuweka wazi, na kwamba
sasa amerudi kwenye kanisa lake la zamani, la EAGT.
Tags
Emmanuel Mbasha
