Rais Dkt. John Pombe Magufuli,jana tarehe 05 Aprili, 2017 amewaapisha viongozi aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali.
Hafla ya kuapishwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Moja ya viongozi walioapishwa ni Prof. Kitila Alexander Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Prof. Mkumbo aliyekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
mmoja wa wanachama wa chama cha ACT Wazalendo, baada ya kuapishwa
aliongea maneno machache akimshukuru Rais Magufuli kwa kuuona umuhimu
wake na kumteua kuwa katibu katika wizara hiyo.
Aidha amemuhakikishia Rais kuwa ataifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na taifa litarajie matokeo makubwa katika utendaji wake.
“Kazi yetu na jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kuwa sera ya umwagiliaji tunaitekeleza” alisema.
Vilevile aliongeza kuwa katika maisha yake yote akiwa mhadhiri, amekuwa
ni mtu wa kuhoji maswali mbalimbali kwa serikali ili kuhakikisha kuwa
wanafanya kazi yao kwa weledi.
“Maisha yangu yote mpaka hapa nilipo nimetumia muda wangu mwingi kuhoji
na kuuliza maswali hasa kwa serikali. Nimepata fursa sasa ya kushiriki
kikamilifu, badala ya kuhoji nina kazi ya kujibu maswali ya serikali. Mh
rais nakuahidi kuwa nitajibu hoja mbalimbali za serikali” alisema.
Viongozi wengine walioapishwa jana ni pamoja na Dkt. Ave Maria Emilius
Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Mhe. Baraka Haran Luvanda kuwa Balozi wa Tanzania nchini
India, Mhe. Sylvester Mwakinyuke Ambokile kuwa Balozi wa Tanzania nchini
Afrika Kusini na Bw. Charles Edward Kichere kuwa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Tags
Kitila Mkumbo
