Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth
Magufuli leo Sikukuu ya Pasaka, wameungana na Waumini wa Kanisa la
Africa Inland – Tanzania Dayosisi ya Pwani Pastorate ya Magomeni kusali
Ibada ya Pasaka.
Katika Ibada hiyo Askofu wa Kanisa la Africa Inland – Tanzania Baba
Askofu Charles Salalah ameongoza maombi ya kumuombea Mhe. Rais Magufuli
ili aendelee kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza nchi vizuri na
amempongeza kwa kazi kubwa ya kurekebisha mambo yote yasiyofaa nchini
ikiwemo kuwaondoa viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya na kufuja mali
za umma.
“Mhe. Rais unafanya kazi kubwa ya kutumbua majipu, majipu unayoyatumbua
wewe ni majipu madogomadogo yaliyotokana na jipu kuu ambalo ni dhambi za
mwanadamu, na jipu hili lilitumbuliwa na Bwana Yesu, kwa hiyo sisi
Wakristo wenzako na waumini wengine tunakuombea sana na tunakuunga mkono
katika kazi hii nzito ya kutumbua majipu haya madogomadogo ya watumishi
hewa, mishahara hewa, mikopo hewa na mengine mengi” amesema Askofu
Charles Salalah.
Akizungumza katika Ibada hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Wakristo
wa Kanisa la Africa Inland na waumini wa madhehebu mengine ya dini kwa
kuendelea kumuombea na ameomba maombi hayo yaendelee, na piawaiombee
nchi iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na watu wachapa kazi.
Mapema asubuhi Mhe. Rais Magufuli ameshiriki Ibada ya Pasaka katika
Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo katika Parokia ya Oysterbay Jijini
Dar es Salaam ambapo katika salamu zake za Pasaka Askofu Mkuu wa Jimbo
Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema
baraka zilizoletwa na Yesu Kristo aliyefufuka ni kwa ajili ya watu wote
wakristo na wasio wakristo na amemtakia heri Mhe. Rais Magufuli ili
matumaini ya baraka hizo ziwafikie Watanzania wote.
Amemuombea Mhe. Rais Magufuli kuwa imara katika changamoto na machungu
anayokutana nayo katika uongozi akisema “Yesu Kritso akuimarishe na
akutie nguvu ili matumaini tunayoyadhimisha leo yawafikie Watanzania
wote”
Tags
RAIS MAGUFULI

