IKIWA imebaki siku moja kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti mjini
Dodoma, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imefunguka jinsi itakavyoibana
serikali kwa kuwasilisha bajeti ‘hewa’ kwa mwaka huu wa fedha
unaomalizika.
Aidha, kambi hiyo imesema itakutana na kujadili mapendekezo ya serikali
kuhusu ukomo wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2017/18 ambayo imebaini
kwa kiasi kikubwa hayaakisi uhalisia.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliiambia
Nipashe jana kuwa wamesikitika kuona bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa
mwaka huu wa fedha imetekelezwa kwa kiwango kidogo.
Hata hivyo, uongozi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umesema
wabunge wa chama hicho tawala watajadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka
huu na kupitisha bajeti ya mwaka ujao bila kujali lawama zinazoelekezwa
na upinzani kwa serikali.
Nipashe ilitaka kujua kutoka kwa Mbowe mambo ambayo Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni unakwenda kuyasimamia wakati wa vikao vya Bunge la
Bajeti na vipaumbele vya kambi hiyo katika bajeti ya mwaka ujao wa
fedha.
Mbowe alisema kambi hiyo inaendelea vikao vyake vya kujadili bajeti hizo
ya mwaka huu na ujao kwa kina kabla ya kuwasilisha mapendekezo yake na
kuibana serikali bungeni.
Alisema kwa sasa wanafanya uchambuzi wa bajeti inayoelekea ukingoni
kujua imetekelezwa kwa kiasi gani na maeneo yepi hayajatekelezwa na
serikali, sababu za kushindwa kutekelezwa kwa bajeti na funzo inatoa
lake kuelekea bajeti mpya ambayo itakuwa ya pili kuidhinisha na Bunge
chini ya uongozi wa Rais wa tano, John Magufuli.
“Tunasikitishwa kwamba bajeti tuliyopitisha bungeni na inayotekelezwa ni vitu tofauti sana," Mbowe alisema.
"Taarifa ya Waziri wa Fedha na Mipango (Dk. Philip Mpango) wiki
iliyopita (Machi 28) ilionyesha dhahiri kwamba fedha za maendeleo ambazo
zingesaidia kunyanyua sekta nyingi zilipatikana kidogo sana na baadhi
ya sekta hazikupata fedha kutokana na uwezo mdogo wa kiserikali.
“Wakati hali ikiwa hivyo, serikali inasema imeongeza mapato na inakusanya kwa wingi wakati hali hiyo siyo kweli.
“Bajeti ya mwaka 2015/16 ilikuwa ni Sh. trilioni 23 na bajeti ya kwanza ya Rais Magufuli (2016/17) ilikuwa Sh. trilioni 29.5.
Alikuja na mipango mingi, akapandisha bajeti hadi trilioni 29, tulihoji
sana wakati wa mjadala wa bajeti mwaka jana kuwa haiko sawa na serikali
haina uwezo wa kuongeza mapato ya kukidhi vigezo vya bajeti.
"Matokeo yake tukajipangia mipango mingi, tukapanga shughuli za
maendeleo, matokeo yake tukagundua serikali haina fedha na imekopa sana.
Hii inazidi kuongeza mzigo kwa mkulima na Deni la Taifa.”
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), alisema wakati ikijua utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu
umekuwa wa kusuasua, serikali imekuja na bajeti kubwa zaidi ya Sh.
trilioni 31.69 kwa ajili ya mwaka ujao wa fedha.
“Tunaendelea kuwadanganya wananchi katika mambo ambayo tunajua
hatutatekeleza au serikali ije na mpango wa kukopa zaidi. Kukopa siyo
jambo jema la kujisifia kuwa kila siku mnakopa bila mpango,” alisema.
Mbunge huyo wa Hai mkoani Kilimanjaro, alibainisha kuwa utekelezaji wa
bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu wa fedha bado haujafika hata asilimia
40 ya bajeti iliyotengwa hivyo haoni sababu za serikali kuja na bajeti
kubwa zaidi ya Sh. trilioni 32.
“Baada ya kumaliza uchambuzi wetu, tutatoa msimamo wetu wa kibajeti na
mwelekeo wa kisera wa namna gani tunafikiri ni sahihi uchumi wetu
uelekezwe,” alisema Mbowe.
KIPAUMBELE CHA UPINZANI
Mbowe alisema upinzani unakwenda kwenye Bunge la Bajeti ukiwa na kipaumbele cha uchumi wa vijijini na uchumi wa kilimo.
“Hili (kilimo) ni eneo ambalo safari hii kambi ya upinzani tutalipa
kipaumbele katika kila bajeti tutakazowasilisha. Tunaona eneo hili
serikali ya Magufuli imelisahau kabisa, hazungumzii kilimo mahali popote
bali reli, ndege mambo ya usafirishaji tu,” alisema.
Mbowe alisema kambi ya upinzani imeona kuwa kilimo kinagusa asilimia 70
ya wananchi na kitendo cha serikali kutokipa kipaumbele wanakiona ndiyo
sababu kubwa ya kutopungua kwa umaskini nchini.
"Katika mwaka wa fedha uliopita kilimo kilikuwa asilimia 3.4 ya Pato la
Taifa, lakini lilikuwa anguko la asilimia mbili ikionyesha kuwa
kinashuka zaidi wakati kinahudumia wananchi wengi zaidi,” alibainisha.
Mbowe aliongeza: “Kama kilimo kinashindwa kuchangia kwenye Pato la
Taifa, maana yake wakulima wako hoi, na kama serikali haikupeleka fedha
kwa wakulima, umaskini hautaisha nchini.”
KAULI YA CCM
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza, akizungumza jana, alisema
wabunge wa chama chake watajadili na kupitisha bajeti ya serikali kwa
mwaka 2017/18.
Rweikiza alisema wabunge wa CCM wanatarajia kuona fedha zitakazopatikana
zinaelekezwa kwenye miradi inayowagusa wananchi moja kwa moja.
Mbunge huyo wa Bukoba Vijijini mkoani Kagera alisema: “Tungependa fedha
zipatikane, ziende kutekeleza miradi ya wananchi kwenye sekta ya maji,
elimu, afya na mingine. Utekelezaji wa miradi ya maendeleo uwaguse moja
kwa moja wananchi wa kawaida.”
Alisema miradi ya maendeleo itatekelezwa ikiwa serikali itaendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17 ambao Waziri Mpango
ameshakiri umekuwa wa kusuasua, Rweikiza alisema wabunge wanaijua nchi
na uchumi ulivyo.
“Tunapopitisha bajeti, siyo kwamba kuna kapu fulani tutaenda kutoa na
kutumia, bali tunaweka bajeti kwamba tutumie kiasi fulani
kilichoidhinishwa kulingana na upatikanaji wa fedha,” Rweikiza alisema.
“Zikipatikana hiyo kazi inafanyika, kama haijafanyika tunajua ukaguzi
ukifanywa na CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali),
tutajua ilipatikana kiasi gani na ilitumika kiasi gani na kama
haikupatikana, huwezi kumlaumu mtu.”
Machi 28, Dk. Mpango aliwasilisha bungeni bajeti elekezi ya Sh. trilioni
31.69 kwa mwaka ujao wa fedha huku akibainisha changamoto tano
zilizokwamisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka huu.
Waziri huyo alisema serikali ilipanga kutumia Sh. trilioni 11.82 kwa
ajili ya bajeti ya maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 8.702 zilikuwa za
ndani na Sh. trilioni 3.117 ni fedha za nje.
Hata hivyo, Dk. Mpango alibainisha kuwa hadi kufikia Februari mwaka huu,
fedha zilizokuwa zimetolewa ni Sh. trilioni 3.975 ikijumuisha fedha
zilizotolewa kwa Halmashauri, sawa na asilimia 34 ya bajeti yote ya
maendeleo.
“Kati ya kiasi hicho, fedha za ndani zilikuwa Sh. trilioni 3.103 na fedha za nje Sh. bilioni 871.8,” Dk. Mpango alisema.
Waziri huyo alisema kutotekelezwa kwa bajeti hiyo ni pamoja na kuelekeza
sehemu ya fedha kulipia madeni ya miradi ya maendeleo, na kuchelewa
kupatikana kwa misaada na mikopo kutokana na majadiliano na washirika wa
maendeleo kuchukua muda mrefu.
Nyingine ni kupanda kwa riba ya mikopo ya kibiashara katika soko la
fedha kimataifa, matayarisho hafifu ya miradi na mwamko mdogo wa kulipa
kodi hususan uzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs).
BAJETI ‘HEWA’
Kwa mujibu wa Dk. Mpango, katika kipindi cha Julai 2016 hadi Februari
mwaka huu, jumla ya Sh. trilioni 16.152 zilitolewa kwa wizara, idara
zinazojitegemea, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa,
sawa na asilimia 54.68 ya bajeti yote iliyoidhinishwa na Bunge.
Kati ya hizo, Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 12.177 (sawa na asilimia
41.22 ya bajeti yote) zilizotolewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida,
ikijumuisha makusanyo ya Halmashauri Sh. bilioni 126.3.
VIPAUMBELE VYA SERIKALI
Kwa mujibu wa Dk. Mpango maeneo ya kipaumbele kwa mwaka ujao wa fedha ni
ujenzi wa reli, ukamilishaji malipo ya ununuaji ndege tatu za serikali,
mradi wa chuma Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, uanzishwaji wa kanda
maalumu za kiuchumi ambazo ni Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma na Mtwara,
miradi ya gesi asilia, shamba la kilimo na uzalishaji sukari Mkulazi.
Serikali pia inapanga kuendelea na miradi mingine ya kipaumbele ambayo
ni ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja na uendelezaji
wa eneo la viwanda Tamco, Kiwanda cha General Tyre mkoani Arusha, mradi
wa magadi Soda, kuimarisha mfumo wa taifa wa maendeleo ya wajasiriamali,
na uendelezaji wa viwanda vidogo na ujenzi wa ofisi za Sido.
Mingine ni kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, mazingira wezeshi
kwa uendeshaji biashara, kuimarisha mitaji na kutumia benki za ndani za
maendeleo TIB na TADB, na kuhamishia shughuli za Serikali Kuu makao
makuu Dodoma ambapo tayari wizara zimeelekezwa kutenga fedha.
VIBANO
Katika mkutano ujao wa Bunge, serikali inatarajiwa kubanwa kutoa maelezo
kuhusu kutotekelezwa kwa mpango wa kutoa Sh. milioni 50 kwa kila
kijiji/ mtaa. Ofisi ya Waziri Mkuu iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni
59 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kutekeleza ahadi hiyo ya Rais Magufuli.
Serikali pia inatarajiwa kubanwa na Bunge kutokana na kutotoa ajira kwa
wananchi na pia kutolipa malimbikizo ya madeni ya watumishi wa umma.
Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliahidi
kutoa ajira 71,496.
Kibano kingine ni kwenye miradi ya maji, ujenzi wa meli mpya Ziwa
Victoria na ukarabati wa meli zilizopo kwenye maziwa makuu, uhaba wa
dawa, vifo cya uzazi na utapiamlo, ongezeko la watu nchini, ahadi ya
zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata, ufufuaji wa Kiwanda
cha General Tyre na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Serikali pia inatarajiwa kubanwa ili kutoa maelezo ya kina kuhusu
kitendo cha wizara sita kuweka ofisi kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udom), utekelezaji wa ununuzi na ugawaji wa pikipiki kwa Waratibu Elimu
Kata wa mikoa 18 na kuchangia mafuta kwa ajili ya magari na pikipiki
hizo.
Kibano kingine kwa serikali kinatarajiwa kuwa faida ya mradi wa mabasi
yaendayo haraka, ujenzi wa nyumba za walimu na watumishi wengine wa umma
na uzingatiaji wa sheria ya manunuzi ya umma katika ununuzi wa ndege
mpya za serikali.
Tags
Freeman Mbowe
