Rapa Ney wa Mitego Jana alijikuta katika mvutano na mtu anayesadikika
kuwa ni Askari Kanzu baada ya kumpiga picha za Video yeye na gari lake
bila idhini yake katika kituo cha polisi cha Osterbay Jijini Dar es
salaam.
Tukio hilo liliibuka wakati Ney akiwa ni miongoni mwa watu waliofika
katika kituo hicho kusubiri hatma ya msanii Roma Mkatoliki na wenzake
waliokuwa wakihojiwa kufuatia tukio la kutekwa kwao na kupatikana.
Ney alimng’ang’ania mtu huyo aliyekuwa anamrekodi yeye na gari lake,
ambapo mvutano huo ulishuhudiwa pia na waandishi wa habari wengine
waliokuwa wametanda katika eneo hilo na ulimalizika baada ya mtu huyo
anaesadikika kuwa ni askari kukubali kufuta picha zote alizochukua.
Katika hatua nyingine, Ney alieleza kuwa hakuweza kula kwa siku mbili
tangu alipopata taarifa za kutekwa kwa Roma na wenzake hadi alipopata
taarifa za uhakika jana kuwa wamepatikana.
Baada ya tukio hilo Mama mzazi wa msanii Moni ambaye ni miongoni mwa
waliotekwa na kupatikana, Fatma Saleh Awadhi alisema kuwa amesikitishwa
sana na kitendo alichofanyiwa mwanae na kuongeza kuwa hataki tena mwanae
afanye muziki.
Hata hivyo, Roma alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa wako
salama kiafya na kuahidi kuelezea tukio hilo kiundani zaidi siku ya
jumatatu
Tags
Nay wa Mitego
