BANDA MEDIA BLOG

RAIS WA TTA AWATAKA WATANZANIA KUIPA MSAADA TIMU YA TENNIS YA WALEMAVU INAYOSHIRIKI MICHUANO YA DUNIA


TENISI WALEMAVU
RAIS wa chama cha Tennis nchini (TTA), Denis Makoi amewataka watanzania kujitokeza na kuipa msaada timu ya taifa ya Tennis ya walemavu ambayo inatarajia kwenda kushiriki fainali za dunia nchini Japan.

Akizungumza na Tovuti hii Jijini Dar es Salaam mapema hii leo, Makoi amesema timu hiyo inatarajia kuanza safari ya kuelekea nchini Japan Aprili 29 mwaka huu, lakini bado zipo changamoto mbalimbali zinazoikabili timu hiyo.
Amesema timu hiyo imepata nafasi ya kwenda kuliwakilisha bara la Afrika katika mashindano hayo ya Dunia na ili kufanikisha afari yao ya kwenda nchini Japan wanahitaji zaidi ya Tsh. Milioni 50 zitakazowasaidia katika siku zote za mashindano.
“Najua yapo mashirika, watu na makampuni mbalimbali nchini ambayo yanauwezo wa kuichangia timu yetu hii inayotarajia kwenda nchini Japan na hapa ningependa nisisitize kitu kimoja kwa wadau wenye mapenzi mema na mchezo huu kwamba kama watawasaidia hawa wachezaji wetu kwenda huko nchini Japan basi ushindi lazima urudi nchini,” amesema Makoi.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu hiyo,Riziki Salum amesema tarayari wachezaji wanaotarajia kwenda Nchini Japan wameshaingia kambini kwa ajili ya kuendelea na mazoezi mbalimbali yatakayowasaidia kuibuka na ushindi katika mashindano hayo makubwa duniani.
Amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri ya kujiandaa na michuano hiyo na wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa timu nyingine zitakazoshiriki michuano hiyo ya kimataifa.
“Timu yetu inatarajia kusafiri na wachezaji wanne pamoja na mimi Kocha bila kusahau viongozi wa TTA pamoja na waandishi wa habari hivyo tunawategemea watanzania watusaidie katika hili kwa kutupatia michango yao kwa kiasi chochote watakachokuwa nacho,” amesema Salum.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG