
SERIKALI ya Marekani imesema itaendelea kutoa misaada ya kiuchumi,
ustawi wa jamii na kisiasa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
ili kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili.
Msimamo huo umeelezwa katika ziara ya ujumbe wa Serikali ya Marekani
uliotembelea Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kwa ajili ya kuzungumzia
masuala ya sera za kiuchumi, kisiasa na kijamii huko Ofisi Kuu
Kisiwandui Unguja.
Marekani ambayo ni Taifa kubwa lililoendelea kiuchumi, kijamii na
kiulinzi, imesema kasi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu
ya Saba Zanzibar, linaishawishi taifa hilo kutoa misaada binafsi na
inayopitia katika ngazi za kimataifa, ili kuenzi kwa vitendo juhudi
hizo.
Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Ofisa wa kusimamia Masuala ya Sera za
Kijamii na Kisiasa katika Ukanda wa Nchi za Afrika zilizomo katika
Jangwa la Sahara, Gregory Simpkims alieleza kwamba CCM iimekomaa kisiasa
na inaendelea kuimarika, tofauti na vyama vya kisiasa vya nchi nyingine
barani Afrika, ambavyo baadhi yao vimeanza kupoteza nguvu na kuondolewa
madakarani na vyama vya upinzani.
“Pia tunaamini kuwa vyama vya siasa vilivyopo Zanzibar vitaendelea
kulinda amani ya visiwa vya Zanzibar ili viwe sehemu tulivu
inayoshawishi kila taifa kufanya utalii na shughuli nyingine za
kijamii.”
Pia ujumbe huo ulitaka kujua njia na sera zinazotumiwa na CCM kuendelea
kuaminiwa na wananchi wa Tanzania na Zanzibar, hali inayosababisha
kuimarika kwa uchumi wa nchi hiyo.
Alisema kwamba ujumbe huo ulitaka kujua mambo mbalimbali yakiwemo suala
la Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, siri ya kuimarika kwa CCM
kisiasa na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na ustawi wa kiuchumi wa
Taifa la Marekani na sera za nchi za nje za taifa hilo kwa upande wa
Zanzibar.
Alisema walizungumzia uimarishaji wa sera za kibiashara na kiuchumi ya
nchi za Afrika, ambayo ni Mpango wa Fursa za Kiuchumi za Afrika nchini
Marekani (AGOA), na kueleza kuwa kwa sasa wapo tayari Zanzibar kunufaika
na mpango huo ili bidhaa zake zikauzwe katika soko hilo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdalla Juma
Saadalla maarufu kama Mabodi, alisema ujumbe huo ulihoji kwa nini
taarifa ya wasimamizi wa kimataifa wa uchaguzi wa mwaka 2015, ilikuwa
tofauti na taarifa iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).
Alifafanua kwamba jawabu la swali hilo, lilikuwa ni kwamba CCM inaamini
na kuunga mkono taarifa na maelekezo ya Tume hiyo, kwani ndio iliyokuwa
ikisimamia shughuli za uchaguzi tangu awali.