
MBUNGE wa Kwimba, Mwanza, Shannif Mansour (CCM), anatuhumiwa kugoma
kulipa kodi ya eneo lake la ardhi lenye ukubwa wa hekta 39,000, kiasi
cha zaidi ya Sh. 500 milioni tangu mwaka 2010.
Mansour kupitia kampuni yake ya Sineji Tanzania Limited, anatuhumiwa
kuigomea serikali kulipa kiasi hicho cha fedha kwa madai yeye hawezi
kulipa fedha hizo kwa kuwa anafahamiana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Makazi, William Lukuvi.
Eneo hilo la Mansour na kampuni yake inayojihusisha na utengenezaji wa
malighafi za ujenzi ikiwemo kusaga kokoto, lililopo kata ya Buhongwa,
Nyamagana pia baadhi ya wananchi wanalalamika kulaghaiwa fedha za fidia
za maeneo yao.
Tangu kipindi hicho, mbunge huyo alikuwa anadaiwa kiasi cha Sh. 529
milioni na Halmashauri ya jiji la Mwanza na kwamba wakati alipotakiwa
kulipa fedha hizo tangu mwaka 2010 alikuwa akigoma kulipa fedha hizo kwa
kutumia mwamvuli wa nafasi yake ya ubunge.
Madai ya mbunge huo kuigomea serikali kulipa kodi hiyo, yaliibuliwa jana
na Waziri Lukuvi, wakati alipokuwa akizungumza na wakuu kitengo cha
idara ya ardhi na wakuu wa vitengo vingine katika Jiji la Mwanza.
Akizungumza katika kikao hicho, Lukuvi amesema kuwa anashangaa kusikia
mbunge huyo akigoma kulipa fedha hizo huku watendaji wa halmashauri hiyo
wakishindwa kuchukua hatua za haraka ili kada huyo wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) alipe kodi ya serikali.
Amesema kuwa katika ulipaji wa kodi wa ardhi watumishi wa idara hiyo
wanapaswa kuacha kuangalia kabila wala chama cha mtu kwani waziri hana
mamlaka ya kufuta utaratibu wa ulipaji wa kodi lazima ufuatwe.
Hata hivyo, amesema kuwa watumishi hao wanapaswa kuhakikisha ifika Mei
2, mwaka huu wawe wamemchukulia hatua ikiwemo kuangalia utaratibu wa
kufuta hatimiliki ya mbunge huyo ili waweze kumuuzia mtu mwingine na
kupata mapato.
“Nusu ya lengo lenu la ukusanyaji wa mapato unachangiwa na mtu mmoja
(Mansour), haiwezekani mtu mmoja akatae kulipa kiasi hicho cha fedha na
nyie mnachelewa kuchukua hatua, utaratibu wa sasa hakuna atakayeshindwa
kuchukuliwa hatua kama atashindwa kulipa kodi.
“Eneo lenye ukubwa wa hekta 39,000 sawa na hekari 96, mtu anakataa
kulipa kodi, naagiza ikifika, Mei 2, mwaka majibu ya suala hili yawe
yamepatikana mara moja, mbunge gani ambaye hataki kulipa kodi,” amesema
Lukuvi.
Lukuvi amesema kuwa watendaji wa ardhi jijini hapa, wamekuwa wakishindwa
kuwadai kodi wafanyabiashara wakubwa na badala yake wamekuwa
wakikusanya kutoka kwa watu wa chini na kuagiza tabia hiyo kukoma.
Afisa Ardhi Mteule Jiji la Mwanza, Silvery Salvatory, amesema kuwa
tayari wameisha mchukulia hatua ikiwemo kumfikisha katika baraza la
usuruhishi la ardhi mkoani hapa na uamzi wake unatarajiwa kutolewa Mei
5, mwaka huu.
Tags
CCM