Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishina Simon Sirro
amesema kupotea (kutekwa) kwa msanii Roma Mkatoliki na wenzake ni jambo
la kawaida huku akisitiza kuwa hayajaanza kutokea leo kwani ni tukio
kama matukio mengine.
Kamanda Sirro amesema hayo baada ya kelele za watu kwenye mitandao ya
kijamii ndani ya siku tatu, huku wasanii, wanasiasa pamoja na wadau
mbalimbali wa muziki kuja juu juu ya suala la kupotea vijana hao katika
mazingira ya kutatanisha huku wengine wakihusisha tukio hilo na masuala
ya kisiasa yanayoendelea nchini.
“Matukio ya utekaji hayajaanza leo, hili la kina Roma na wenzake ni
tukio kama matukio mengine yaliyokuwa ya ujambazi kwa hiyo tupeni muda
tupeleleze, tukifika mahali pazuri tutawaita tuwape taarifa lakini
nimeona mitandao mingi inazungumza, jana nikaona wasanii wamekutana
lakini nikajiuliza hivi yangekuwa haya matukio yanatokea ya uhalifu
yanapotokea watu wanakutana ingekuwaje ?,Jamani kazi hii tumepewa kwa
mujibu wa Katiba na ni lazima tutimize wajibu wetu kwa hiyo tupeni muda
tutakuwa na majibu mazuri katika hili”. Alisema Kamishna Sirro pindi
alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari ofisni kwake Jijini Dar es
Salaam
Aidha Kamanda huyo amesema mpaka sasa wameshaunda timu ya uchunguzi na
inaendelea vizuri katika upelelezi huku akiwataka wananchi kuwa na subra
kwa kuwa upelelezi ndiyo utasema kila kitu.
Kwa upande mwingine amewataka watu waache tabia ya kujifanya wao ndiyo
‘Kamishna Sirro’ na kutaka kuzungumzia habari za upelelezi hivyo
amewataka watu kuliamini jeshi la Polisi kwa kuwa hawapendi vitendo
hivyo viwepo na viendelee kutokea.
