Timu
ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 maarufu
kama Serengeti Boys, inatarajiwa kusafiri kesho saa 10.45 jioni kwa
Ndege ya Shirika la Ndege la Emirates kwenda Morocco kupitia Dubai,
Falme za Kiarabu (UAE).
Timu
hiyo yenye wachezaji 23 na viongozi wanane watakuwa Uwanja Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere kuanzia saa 7.00 mchana kwani
wanatakiwa kuanza kuingia uwanjani saa 7.45 kwani saa tatu baadaye
ndipo ndege itakapopaa.
Wanahabari
wanaweza kupata mahojiano ya mwisho kadhalika kupata picha za habari
wakati huo wa mchana kabla hawajaingia ndani kwenye ukaguzi wa taratibu
za (check in logistics).
Kabla
ya kusafiri, timu hiyo ilikuwa kambini hapa nyumbani tangu Januari 29,
mwaka huu na baada ya kambi ya mwezi mmoja na nusu, ilicheza mechi tatu
za kirafiki za kimataifa.
Machi
30, 2017 ilicheza Burundi ‘Intamba Murugamba’ na kushinda mabao 3-0
kabla ya kurudiana tena Aprili 1, mwaka huu na kushinda mabao 2-0. Mechi
zote mbili zilifanyika Uwanja wa Kaitaba, ulioko Bukoba mkoani Kagera.
Mechi
ya mwisho hapa nyumbani ilifanyika Aprili 3, mwaka huu dhidi Ghana
‘Black Starlets’ na kutoka sare ya 2-2 katika mchezo ulifanyika Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Serengeti
Boys ilitumia mchezo kama ishara ya kuwaaga mamilioni ya Watanzania
kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.
Serengeti
Boys itakuwa Rabat, Morocco kufanya kambi ya takribani mwezi mmoja
kuanzia Aprili 5, mwaka huu. Ikiwa huko angalau itacheza mechi za
kirafiki zisizopungua mbili dhidi ya wenyeji morocco na timu nyingine ya
jirani ama Tunisia au Misri.
Kambi
hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu itasafiri
hadi Cameroon. Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili za kirafiki za
kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu kabla ya kusafiri
Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys imepangwa kundi B
pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
Tags
SERENGETI BOYS