Jeshi la Polisi Tanzania limesema limewaua majambazi wanne ambao
walikuwa ni sehemu ya kundi la majambazi lililowashambulia na kuwaua
askari 8 wilayani Kibiti mkoani Pwana jana usiku.
Akizungumza na wanahabari leo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa
jeshi hilo, Nsato Marijani amesema kuwa mara baada ya kundi hilo
kuwashambulia askari, kikosi kingine cha askari kilifanya msako na
kubaini maficho ya majambazi hao.
Amesema baada ya kuwabaini, yalifanyika mashambulizi ya kurushiana
risasi, ambapo majambazi wanne waliuawa pamoja na kukamata bunduki 4
zikiwemo SMG mbili zilibainika kuwa kati ya zile zilizoporwa na
majambazi hao.
Akielezea tukio hilo lilivyokuwa, Kamishna Marijani amesema kundi la
waharifu walikuwa na silaha za moto na ambao idadi yao haikujulikana
liliweka mtego na kufanikiwa kuishambulia kwa risasi gari iliyokuwa na
askari 9 waliokuwa wakitoka katika malindo kurudi kambini, na kuwaua
askari 8 kati yao huku mmoja akijeruhiwa mkononi.
Amewataja askari waliuawa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter
Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC
Maswi na PC Ayoub, ambapo pia walipora bunduki 7 zikiwemo SMG 4.
Kufuatia tukio hilo, Kamishna Marijani ametangaza vita na waharifu wote
katika maeneo hayo, ambapo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaanza
oparesheni maalum katika mkoa wa Pwani, kuhakikisha vinawasaka na
kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua.
Mpaka sasa jeshi limekwisha poteza skari zaidi ya 10, inatosha….
Tunakwenda kweny oparesheni maalum, hatutakuwa na mzaha, tutawasaka
popote walipo na kuwashughulikia kikamilifu, ,,, watajua tofauti ya moto
na maji… mpaka jana idadi ilikuwa ni 8 kwa nne, lakini nawahakikishia
kuwa ndani ya wiki moja idadi hiyo itakuwa imebadilika, na tutakuwa na
hesabu tofati” amesema Marijani
Kuhusu hofu ya ugaidi, Kamishna Marijani amesema tukio hilo siyo la
kigaidi bali ni uhalifu wa kawaida, huku akibainisha kuwa Tanzania
hakuna ugaidi
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limepiga marufuku uendeshaji wa
pikipiki katika maeneo yote ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji zaidi ya saa
12:00 jioni. Amesema usafiri wa boda boda utaruhusiwa kati ya saa 12:00
asubuhi hadi saa 12:00 jioni
Tags
Jeshi la Polisi