Ametoa agizo hilo leo jioni
(Jumatano, Aprili 6, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati akitoa maelezo ya
kuhitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake
na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja
ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe ambaye
aliitaka Serikali itoe maagizo kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri
kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali
inayotekelezwa katika Halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa
agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.
“Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa
Mbunge kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015,
Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini
kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo ya
ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa ajira kila robo
mwaka,” amesema.
Waziri Mkuu amesema maelekezo
hayo, yanazingatiwa katika Mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali
unaotolewa na HAZINA kila mwaka ambao unazitaka Mamlaka za Serikali za
Mitaa, Wizara na Taasisi zote zibainishe fursa za ajira zinazotarajiwa
kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Vilevile mwongozo huo unazitaka
taasisi hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na
utekelezaji wa miradi hiyo kila robo mwaka. Ninatoa agizo, Mamlaka ya
Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi zote ziendelee kuzingatia maelekezo
haya,” amesema.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa
viwanda, Waziri Mkuu amesema ndani ya mwaka mmoja, jumla ya viwanda
2,169 vimesajiliwa vikiwemo viwanda vya mbolea, saruji, chuma na vya
usindikaji wa mazao.
“Serikali pia inaendelea
kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia uwekezaji nchini. Uhamasishaji
wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na tayari tumeanza kuona matokeo.
Kwa mfano, mkoa wa Pwani peke yake una viwanda vikubwa 83 na vingine
vidogo vidogo zaidi ya 200. Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya
Tano,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye
Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama alisema Programu ya Miundombinu ya
Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) ilipanga
kukarabati barabara zenye jumla ya kilomita 148.5, kujenga masoko manne
na kukarabati kituo kimoja cha mafunzo ya utunzaji mazao baada ya
kuvuna.
Akijibu hoja za utekelezaji wa
programu hiyo kwa upande wa Pemba na Unguja, Waziri Mhagama alisema
miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ilianza Agosti na Novemba 2014
na kazi hiyo kwa Pemba ilikamilika Desemba 2015 wakati kwa upande wa
Unguja ilikamilika Januari 2016.
“Kazi za ujenzi wa masoko ya
Kinyasini na Mombasa (Unguja) pamoja na Konde na Tibirinzi (Pemba)
zilianza Desemba 2016 na zinatarajiwa kukamilika Julai 2017.
Wakandarasi wamehimizwa kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo katika muda
uliopangwa ili kuendana na ratiba iliyopangwa,” alisema.
Akijibu hoja kuhusu uamuzi wa
Serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mhagama alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma
na kuifanya Makao Makuu ya Serikali ilikuwa ni ndoto ya Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alitaka kuona Dodoma ikistawi na
Serikali kuweza kuhamia huko ili kutekeleza kwa vitendo dhana ya Mji
Mkuu.
Alisema uamuzi wa Serikali
kuhamia Dodoma siyo suala la kisiasa kama baadhi ya watu wanavyodai bali
ni utekelezaji wa maamuzi kamili kama yalivyoelekezwa kwenye Ibara ya
151 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 na kama ilivyotamkwa
kwenye GN namba 273 ambayo ni tamko la Serikali na sheria halali.
Naye Naibu Waziri wa Kazi, Ajira
na Vijana, Mhe. Anthony Mavunde alisema kila mwaka vijana kati ya
800,000 hadi milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira wakati soko la
ajira ni dogo.
Hata hivyo, Naibu Waziri Mavunde
alisema Serikali imeanza kubadilisha mtazamo wa vijana kuhusu ajira
kwani wengi wao hudhani kwamba kuwa na ajira ni lazima mtu avae tai, awe
na ofisi yenye meza na kiti kinachozunguka.
Tags
WAZIRI MKUU MAJALIWA