Mchezo wa Robo Fainali ya Nne
ya Kombe la Shirikisho la Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017),
kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC utafanyika kesho Aprili
22, 2017 saa 10.00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo utatoa mshindi
ambaye ataungana na timu nyingine tatu ambazo tayari zimefuzu kwa hatua
ya Nusu Fainali. Timu zilizotangulia Nusu Fainali ya ASFC ni za Mbao FC,
Simba SC na Azam FC.
Jumapili Aprili 23, mwaka huu
kutakuwa na droo ya wazi kwa timu nne zitakazokuwa zimefuzu kwa hatua ya
Nusu Fainali ya ASFC, itakayofanyika Kituo cha Televisheni cha Azam
ambao ni wadhamini wakuu wa jina la michuano na haki ya kuonesha
mubashara michuano hii ambayo inafanyika kwa msimu wa pili mfululizo.
Azam FC ilikata tiketi ya
kucheza Nusu Fainali ya ASFC baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 3-1,
kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es
Salaam Aprili 5, 2017 ikitanguliwa na Mbao iliyoishinda Kagera Sugar
mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi
18, 2017 ilihali Machi 19, mwaka huu Simba iliwatoa Madini ya Arusha
kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Nusu Fainali inatarajiwa
kufanyika baadaye mwaka huu, kabla ya fainali ambako Bingwa wa michuano
hii ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 ikiwa ni pamoja na za Ligi
Kuu ya Vodacom (timu 16); Ligi Daraja la Kwanza (timu 24); Ligi Daraja
la Pili (timu 24) na mabingwa wa mikoa timu 22, atazawadiwa Sh. 50
milioni na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe
la Shirikisho – CAF.
…………………………………………………………………….………………………
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
Tags
yanga