
Mbunge wa Jimbo la Mtama Mh. Nape Nnauye ameshauri vyombo vya usalama
nchini vitimize majukumu yao pasipo kutumia nguvu sehemu ambayo
mazungumzo yanaweza kuwa na tija ili kuendelea kulinda nchi katika namna
nzuri ya kushirikiana.
Mh. Nape amesema kuwa vyombo vya dola vimekuwa ni vyombo vya wananchi
"Ni vizuri vyombo vya dola vikatimiza wajibu wao na ni vizuri tukalinda
nchi yetu katika mazingira ambayo tumekuwa tukihusiana kwa muda mrefu,
vyombo hivi vya dola hivi vimekuwa ni vyombo vya wananchi na ndio maana
jeshi letu linaitwa jeshi la Wananchi wa Tanzania, si vizuri kutumia
nguvu kubwa pale ambapo hapahitajiki kutumia nguvu kubwa. Na mimi
nimeendelea kushauri nchi yetu bado tumeendelea kufanya mambo yetu kwa
mazungumzo kwa kuelewana" alisema Nape Nnauye
Mbali na hilo Nape Nnauye anasema mambo haya ya polisi kutumia nguvu
sehemu isipohitajika nguvu yanajenga chuki kati ya wananchi na serikali
yao.
"Nchi yetu hatukuzoea hayo, nchi yetu hatukuzoea mabavu, kwanza matendo
haya yanajenga chuki kati ya serikali na wananchi, yatajenga chuki kati
ya Rais na wananchi, yatajenga chuki kati ya CCM na wananchi kwa sababu
itafika mahali wananchi hawakuzoea mambo haya watajenga chuki tu kuona
nchi yetu haiendi sawasawa" alisisitiza Nape Nnauye
Tags
Nape Nnauye