
Mfanyabiashara tajiri Afrika, Aliko Dangote anasubiri idhini ya Benki
Kuu ya Nigeria ili anunue kiwanda cha kuunda magari aina ya Peugeot
akishirikiana na majimbo mawili.
Kampuni ya Usimamizi wa Mali ya Nigeria (AMCON), iliyoundwa wakati wa
kuyumba kwa benki, inakaribia kuuza Kiwanda cha Magari cha Peugeot cha
Nigeria (PAN).
“Tumeshakamilisha mchakato wote wa zabuni miezi miwili iliyopita na sasa
tunasubiri idhini ya Benki Kuu,” alisema ofisa mtendaji mkuu wa AMCON,
Ahmed Kuru alipoongea na Reuters.
PAN, kiwanda cha kuunda magari kilichopo jimbo la Kaduna, kina ubia wa
kiufundi na PSA Peugeot Citroen na kikiwa na uwezo wa kuunganisha magari
90,000 kwa mwaka.
Dangote, kwa kushirikiana na majimbo ya Kaduna na Kebbi na Benki ya
Viwanda (BOI) waliomba zabuni ya kuwa wamiliki wakubwa wa hisa za PAN
mwaka jana kutokana na AMCON kutaka kuuza baadhi ya mali zake
ilizozichukua wakati wa matatizo ya taasisi za kifedha.
Tags
Dangote