
Ulimi ni kiungo muhimu sana kwenye maisha ya binadamu. Neno moja
linaweza kujenga au kubomoa ukuta mkubwa wa ndoa uliojengwa kwa gharama
kubwa ya uvumilivu, uaminifu na upendo.
Hivyo, ni jambo muhimu sana kukumbushana japo kwa machache baadhi ya
sentensi zinazotumika mara kwa mara na kuonekana kuwa za kawaida, lakini
zinaweza kuwa chanzo cha kuvunja ndoa au kuvuruga uhusiano
uliostawishwa kwa gharama kubwa.
Leo nitagusia sentensi tatu za kawaida kabisa ambazo hutumiwa na baadhi
ya wanawake bila kufahamu kuwa zinaweza kuwa chanzo kikuu cha kuutafuna
uhusiano wao.
“Mama Yangu Alinionya Kuwa Utanifanyia Hivi.”…
Sentensi hii inaweza kumfanya mmeo kuwaza mengi sana kuliko
ulivyomaanisha wewe pale unapotaka kumkosoa kwa alichokifanya. Kwanza
atagundua kuwa una watu wengi nyuma yako ambao wanakusaidia kumfikiria
‘hasi’.
Kibaya zaidi unapomuweka kwenye kundi hilo mama yako ambaye yeye
anamheshimu sana. Hii linaaweza kupelekea mchumba au mme wako
kutokumuamini mama yako na kuanza kumuona kama adui wa uhusiano wenu.
Unadhani mama yako akiwashauri jambo atalichukuliaje? Hata kama ni zuri.
“Unafikra Kama Za Baba Yako” (Unapomkosoa)
Bila shaka unafahamu ni kiasi gani wanaume huwaheshimu sana na kuwaamini
sana baba zao ambao wamewashauri mengi hadi walipofika hapo. Hata kama
huwa anakueleza baadhi ya fikra au mawazo ya baba yake asiyokubaliana
nayo, usidhubutu kabisa kumtolea mfano kumuonesha kuwa na wewe
unamchukulia hivyo mzazi wake.
Kukosoana ni suala zuri katika maisha ili kurekebishana lakini angalia
njia nzuri ya kupinga hoja ya mwenzi wako, kwa ustaarabu kuepuka
kumkera.
“Hivi Lini Utapata Kazi Mpya..?”
Swali hili sio baya lakini kwa jinsi lilivyoulizwa lina kila dalili za
kuleta shida sana kwenye fikra za mumeo/mchumba wako. Kwanza atajua ni
kiasi gani unafikiria vibaya kuhusu maisha yenu hasa kiuchumi.. Ni bora
kumwambia, “Mume wangu ninakuombea sana upate kazi mpya.” Ni ujumbe
uleule lakini jinsi ulivyofikishwa unatofautiana sana.