
Baada ya staa wa filamu Bongo, Wema Sepetu kuvaa nguo zenye rangi ya
Chama cha Mapinduzi (CCM) alipotinga mahakamani hivi karibuni angali ni
mwanachama damu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kisha
baadhi ya wafuasi kudai anawasaliti, uongozi wa chama hicho umemtolea
tamko.
ILIKOANZIA
Wema hivi karibuni akiwa ameongozana na mama yake, Miriam Sepetu na
mashosti zake wengine, alitinga kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
jijini Dar kwenye ile kesi yake ya ‘unga’ akiwa amevaa gauni refu la
njano, juu akiwa amevaa ‘koti laini’ lenye rangi ya kijani na wekundu
kwa mbali, hali iliyoibua mjadala kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa
mahakamani hapo.
“Huyu mbona leo katuvalia nguo hizi? Hizi si rangi za CCM kabisa? Mh!
Kwa hili siyo sawa kabisa,” alisikika akisema mwanamke mmoja aliyekuwa
amevaa magwanda ya Chadema.
Mwingine akadakia: “Ni kweli rangi siyo ishu lakini kwa yeye ambaye
juzijuzi alitangaza kuwa sasa ni Chadema damu, mavazi ya rangi hizi
angeyachukia, sasa ona, utadhani ni kada wa CCM bwana.”
Kutokana na suala hilo kuibua maswali mengi kwa baadhi ya wanachama wa
Chadema waliokuwa mahakamani hapo, Risasi Jumamosi liliwatafuta baadhi
ya viongozi wa Chadema na kuwauliza kuhusiana na suala hilo ambapo kila
mmoja alitoa tamko lake.
Meya wa Ubungo ambaye ndiye mlezi mkuu wa Wema Sepetu, Boniphace Jacob
alisema; “Chadema siyo nguo, ni imani na itikadi kwani mahakamani lazima
avae sare za Chadema? Hizo ni nguo tu kamanda, siyo ‘big deal’ sana.”
Kwa upande wa msemaji wa chama hicho, Tumaini Makene alieleza; “Hivi
wale mashabiki au wanachama wa Simba wakivaa nguo za njano au kijani kwa
sababu yoyote ile huwa ni ‘puppets’ (vibaraka) wa Yanga? Nadhani majibu
hayo yamejitosheleza.”