
Baada ya kuwepo kwa madai kuwa mastaa wa filamu Bongo, Jacob Steven
(JB), Single Mtambalike (Rich) na Vincent Kigosi (Ray) walihongwa fedha
na viwanja ili ‘kuinjinia’ maandamano ya hivi karibuni kupinga sinema za
nje, mastaa hao wamebanwa na hatimaye kufungukia ishu hiyo
inayowatafuna, Risasi Mchanganyiko lina mkanda kamili.
Chanzo kilicho karibu na tasnia hiyo kililiambia Risasi Mchanganyiko
kuwa kampuni moja ya usambazaji filamu (jina kapuni kwa sasa), iliwapa
fedha baadhi ya waigizaji ili wafanye maandamano ya kuziondoa sokoni
filamu hizo za nje, zinazodaiwa kukingiwa kifua na Rais wa Shirikisho la
Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba.
Inadaiwa kuwa baada ya kampuni hiyo ya usambazaji ‘kupenyeza sumu hiyo’
waigizaji hao walikwenda kwa kigogo mmoja wa kisiasa na kumshawishi
kuwaunga mkono, ambaye naye alikubali na kuwaomba waigizaji hao kufanya
kila wawezalo, kumtoa kwenye kiti chake, Simon Mwakifwamba, kwani ana
ukaribu na hasimu wake wa siasa.
“Kuna watu wamevuta huku na huku katika hii ishu, wale wasambazaji
hawazitaki kabisa filamu za ndani kwa sababu zinaharibu soko lao, ingawa
wana kisingizio cha kodi, hawana lolote, watu hawataki sinema za Bongo
kwa sababu hazina ubora,” kilisema chanzo hicho.
Kiliendelea kudai kuwa katika kuhakikisha lengo hilo linafanikiwa,
kigogo huyo wa kisiasa anadaiwa kutoa hongo ya viwanja kwa mastaa hao,
ambavyo vinadaiwa viko Kigamboni jijini Dar.
Ili kuujua ukweli juu ya tuhuma hizo, Risasi Mchanganyiko liliwatafuta waliotajwa na kuwabana ili wafungukie ishi hiyo.
Ray alipoulizwa alijibu akisema; “Hiyo ishu ya kupewa viwanja hainiingii
akilini, kwanza ili iweje, mimi nilienda kwenye maandamano maana ni
ishu iliyokuwa inanihusu kama msanii wa filamu, huyo Mwakifwamba ambaye
anapinga suala hilo atakuwa ana mambo yake ya kisiasa, kwanza yeye mara
ya mwisho kutoa filamu sijui ni lini.
“Sisi tunapigania haki yetu maana filamu za nje hazitozwi kodi, ndiyo
maana zinauzwa bei rahisi kitu ambacho kinaathiri soko la filamu zetu
nzuri na zenye ubora tunazozitengeneza.”
Kwa upande wa JB alipoulizwa kuhusiana na hilo alijibu; “Ili iweje?
Kwani (anamtaja kigogo huyo) anapata wapi viwanja? Uongo huo wa kijinga.
Mimi nilienda pale kushiriki maandamano kwa sababu ni mdau, si
vinginevyo.
“Hebu fikiria, hivi unaona tofauti za bei za bia? Bia za nje na ndani
ziko sawasawa? Zinatofautiana kwa sababu ya kodi na ili kulinda viwanda
vya ndani,” alisema muigizaji huyo maarufu.
Kwa upande wa Rich, naye kama walivyo wenzake, alisema madai ya kupewa
hongo ya viwanja na fedha ni ya uongo, kwani yeye alianza kushiriki
kampeni za kukamata filamu za nje tangu enzi zile Nape Nnauye akiwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
“Kwanza mimi siyo timu (kigogo), nilienda pale kama mdau na wala
sikwenda pale kupinga kazi za nje, nilienda pale kutaka filamu zote
zilipe kodi. Tatizo la filamu zetu siyo zile za nje, bali ni ubovu wa
kazi zetu.
“Kama tutatengeneza kazi nzuri zitauzika tu sokoni, lakini kama kila mtu
mwenye fedha anadhani anaweza kutengeneza filamu, hiyo ndiyo
inayoharibu soko letu. Ninakubali kuna udhaifu katika filamu za ndani,
ambazo nadhani ndiyo zinachangia kuua soko, si filamu za nje,” alisema.
Tags
Bongo Movies