Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe
amepiga marufuku Runinga na Redio kusoma habari nzima katika magazeti
huku akivitaka kusoma vichwa vya habari tu.
Dkt. Mwakyembe ametoa agizo hilo, jijini Mwanza ambapo amesema
kutekelezwa kwake kunaanza kesho (Alhamisi) tarehe 04/05. Leo ikiwa ni
siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, Mwakyembe amesema ataendelea
kutetea na kulinda haki za waandishi wa habari huku akiwahakikishia
ulinzi katika kazi zao.
Mwakyembe amesema amepiga marufuku kusomwa kwa magazeti kwenye runinga
na redio, ili magazeti yaweze kuuzwa kwani punde habari yote inaposomwa
kwenye chombo cha habari na watu wakasikiliza maeneo yote, hakuna mtu
atakayenunua gazeti hilo.
