
Pengine tayari unafahamu kuwa kutokujishughulisha na mazoezi ya viungo
mara kwa mara ni hatari kwa afya yako. Ndiyo hilo ni jambo ambalo kila
mtu analijuwa (common sense). Vipi lakini ikiwa ni kweli unajitahidi
kila siku kutimiza jukumu hilo la kufanya mazoezi dakika 30 hadi lisaa
limoja na wakati huo huo unatumia masaa mengi ukiwa umekaa kwenye kiti,
ukiangalia TV masaa mengi, masaa mengi umekaa na una kazi katika
Kompyuta?.
Ndiyo wewe unadhani kwakuwa unaenda kufanya mazoezi kila siku basi hiyo
inatosha, si ndiyo?. Ukweli ni kuwa hata kama wewe ni mtu wa
kutembeatembea hapa na hapa lakini kama masaa mengine mengi yanatumika
ukiwa umekaa kwenye kiti, mwili wako unakuwa karibu na magonjwa mengi
bila mwenyewe kutambua.
Haya ndiyo madhara 7 ya kiafya utakayoyapata ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa masaa mengi kwenye kiti au chini kila siku:
1. Kunakosesha kupata oksijeni ya kutosha
Mara nyingi ukiwa umekaa unapenda kuegemea mgongo na siyo kukaa wima
umenyooka, matokeo ya mkao huu ni kuzuia oksijeni kutembea kwa uhuru
wote ndani ya mwili na mapafuni kwa ujumla.
Kisayansi tunapumua kwa uhuru wote tukiwa tumesimama na siyo tukiwa
tumekaa. Ukiwa umesimamaa ndipo mapafu hupata uwezo wa kujitanua mpaka
mwisho na hivyo kuweza kutoa hewa chafu na kuingiza hewa safi ndani
kiurahisi zaidi. Hali hii ya kukosa oksijeni ya kutosha mwilini
hujulikana kwa kitaalamu kama ‘hypoxia’. Wanasema kukaa kwenye kiti
masaa matatu tu ni sawa na mtu aliyevuta sigara 6. Bila kupata oksijeni
ya kutosha mwilini mwako kunapelekea magonjwa mengi mwilini bila idadi.
2. Unapata kirahisi kansa ya titi na kansa ya tumbo
Kansa ya titi na kansa ya utumbo mpana mara nyingi imeonekana kujitokeza
kwa watu wa kula kulala yaani wale wasiopenda kujishughulisha na
mazoezi ya viungo. Kituo cha kudhibiti magonjwa cha Marekani (CDC)
kimesema maisha ya kula kulala yanaweza kukuweka kuwa karibu karibu na
kansa kwa zaidi ya 40%. Hii ndiyo sababu wanawake wengi wanapatwa na
kansa ya matiti miaka hivi karibuni sababu wengi wao ni watu wa kukaa tu
nyumbani masaa mengi tofauti na wanaume ambao hutembea huku na huko
kutafuta riziki ya kila siku. Kuepuka kansa ya matiti na kansa ya utumbo
mpana epuka kukaa kwenye kiti masaa mengi.
3. Una uwezekano mara 147 zaidi wa kupatwa na maradhi ya moyo
Matatizo katika mfumo wa upumuwaji ndiyo moja ya matokeo makubwa unaweza
kuyapata ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa kwenye kiti masaa mengi. Ni
matokeo ya kutokupata oksijeni ya kutosha kama matokeo ya kukaa kwenye
kiti masaa mengi. Kwenye utafiti mmoja uliohusisha watu 800,000, wale
waliokuwa wakikaa kwenye kiti masaa 10 kila siku walikuwa na uwezekano
mara 147 zaidi wa kupatwa na magonjwa ya moyo kuliko wale waliokaa
kwenye kiti masaa machache au mara moja moja.
Kuna tafiti nyingi zinazokubaliana na nadharia hii na inatokana na
ukweli kwamba ukiwa umekaa ni rahisi mafuta mengi kujilundika mwilini
mwako kuliko ukiwa umesimama. Kadri unavyokaa masaa mengi kwenye kiti
ndivyo vimeng’enya vinavyofanya kazi ya kuchoma mafuta mwilini
vinavyokuwa na nguvu chache kuchoma hayo mafuta. Na tatizo la unene au
uzito kupita kiasi lina uhusiano wa moja kwa moja na matatizo mbalimbali
ya moyo.
4. Itakuwa vigumu kitambi na uzito kukuisha
Umewahi kujaribu kufanya mazoezi, kubadili chakula au hata kufunga na
bado ukawa unasumbuliwa na kitambi au uzito kuwa mkubwa? Basi jibu la
tatizo lako ni kukaa kwenye kiti masaa mengi. Utafiti unaonyesha kukaa
tu kwenye kiti hata kama hauli chakula kingi bado utaendelea kuongezeka
uzito.
Kwahiyo kama unataka kuondoa kitambi au tumbo au kupungua uzito kwa
haraka acha kukaa masaa mengi kwenye kiti, hata kama kazi yako ni ya
ofisini jaribu namna unaweza kupata meza ya kusimama huku unaendelea na
kazi yako.
5. Ni rahisi kupatwa na ugonjwa wa Kisukari
Unataka kupona au kuepukana na Kisukari aina ya pili? Basi acha kukaa
kwenye kiti muda mrefu. Moja ya hatari zaidi za kukaa kwenye kiti masaa
mengi ni kuwa mwili unakuwa hauitiki vema kwa insulin jambo ambalo ni
matokeo ya kukaa masaa mengi kwenye kiti na hii ni matokeo ya kuzalishwa
kwa wingi kwa kongosho kupita inavyohitajika kama matokeo ya kukaa muda
mrefu.
Wakati ukiwa umekaa tu kwenye kiti kongosho linaendelea kutengeneza
insulin lakini katika mwili huo uliokaa tu, insulin inakuwa haitumiki
vema na mwili jambo linalomaanisha kuwa damu sukari (glucose)
haiondolewi kwenye mzunguko wa damu kwa haraka. Hivyo uwezekano wa
kupata Kisukari unaongezeka kwa zaidi ya asilimia 14 kwa Yule mwenye
tabia ya kukaa masaa mengi kwenye kiti kuliko mtu mwingine yoyote.
6. Utapatwa na maumivu ya nyuma ya mgongo
Ukiwa ni mtu wa kupenda kukaa kwenye kiti masaa mengi kuna uwezekano
ukawa haukai hata mkao mzuri kiasi cha kuwa karibu na maumivu ya mgongo
kila mara. Watu wa namna hii pia huwa na maumivu ya kwenye uti wa mgongo
kila mara. Kwa mjibu wa utafiti wa Taasisi ya ‘DNA India’ wagonjwa
wengi wenye matatizo ya uti wa mgongo ni wale wenye miaka 20 na 30 na
wengi wao ni wale hufanya kazi wakiwa wamekaa kwenye kiti masaa mengi.
Miaka ya sasa ni rahisi kukutana na watu wanaolalamika kupatwa na
maumivu ya mgongo na wengi wao ukiwachunguza ni wale wanaotumia masaa
mengi kukaa kwenye kiti.
7. Utakufa ukiwa bado kijana
Shirika la afya duniani limesema mtindo wa kukaa masaa mengi kwenye kiti
ndiyo unaohusika na kuongezeka kwa uzito na unene kupita kiasi katika
nchi nyingi zilizoendelea. Na uzito kupita kiasi ni moja ya tatizo kubwa
la afya kwa mtu mzima yoyote kuwa nalo ingawa wengi hawaelewi hilo,
wengi hasa waAfrika wakiwa wanene au wenye uzito mkubwa ndiyo hudhani
hiyo ni afya. Uzito na unene kupita kiasi huja na matatizo mengine
makubwa ikiwa ni pamoja na matatizo katika mfumo wa upumuwaji, kisukari,
stroke, kukosa usingizi nk na haya yote yanaweza kupelekea wewe kufa
ukiwa bado kijana.
Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Harvard mwaka 2014 ulitoa hitimisho
kwamba kukaa kwenye kiti masaa mengi ni moja ya sababu ya vifo vya
mapema kwa watu wengi. Mtandao wa Huffington ulienda mbali zaidi na
kusema kukaa kwenye kiti masaa matatu tu kwa siku ni sawa na mtu
aliyevuta sigara 6 na kuwa kukaa kwenye kiti masaa mengi kunaua watu
wengi zaidi duniani kote kuliko hata UKIMWI.
Mara ya kwanza niliposoma habari hizi nilishikwa na mshangao wa ajabu
maana mimi mwenyewe nimekuwa mtu wa kukaa kwenye kiti kwa miaka mingi
sasa kwani kazi zangu nyingi huzifanya nikiwa kwenye computer. Yaani
haikuchukuwa muda nikabadili mkao tayari ninafanya kazi zangu nikiwa
nimesimama, na tayari nimeona mabadiliko makubwa kwenye afya yangu kwa
ujumla.
Pamoja na kuwa kusimama ni bora zaidi kuliko kukaa, bado unatakiwa
utumie muda fulani kukaa pia, usisimame masaa yote kutwa nzima,
ukisimama masaa matatu tumia nusu saa nyingine kukaa hivyo hivyo mpaka
siku yako inaisha.
Nini maoni yako? umekaa muda mrefu kwenye kiti na unapata mojawapo ya madhara yaliyoandikwa hapa? nipe uzoefu wako.