
Na Edward Lucas
Utamu wa tendo la ndoa umepewa upekee wa kutolinganishwa na chakula
chochote duniani, lakini kumbukumbu ya tendo hilo hutofautiana sana kati
ya mwanaume na mwanamke. Utanielewa ukiendelea…
Binafsi nakumbuka sana utani wa rafiki yangu tuliyemtania kwa jina la
‘Ngoswe’, ambaye aliwahi kutuambia, “Unajua ni rahisi sana mwanamke hata
aliyezeeka kukumbuka alijisikiaje mara ya kwanza kufanya mapenzi akiwa
na miaka 20 hivi. Lakini ni vigumu sana kwa mwanaume aliyefanya mapenzi
mara kadhaa, kukumbuka vizuri utofauti aliousikia alipofanya tendo hilo
kwa mara ya kwanza.”
Ngoswe alitumia maneno yenye ukakasi kunilazimisha kuelewa alichokuwa
anazungumzia ili nifahamu kuhusu mahusiano ya mapenzi aliponiona
nimezama katikati ya kina cha penzi la mrembo mmoja aliyeniendesha kama
gari lililokata break kwenye mteremko.
Huyo jamaa alinambia kuwa kinachoshangaza, katika maisha ya uhusiano,
utamfanyia mwanamke kila kitu unachotaka, lakini kumbuka kuwa kwa kiasi
kikubwa kumbukumbu yake hufutika na kurejea upya kana kwamba mmeanza
jana tu. Sikumuelewa hadi yaliponikuta na kujikuta nikishindwa
kusikitika hata kidogo nilipoambiwa kuwa mpenzi wangu ameambukizwa
virusi vya ukimwi.
Najua wengi watashtuka sana kwa neno hili hasa wakijiuliza inakuaje mtu
afurahi wakati mwenzie yuko kwenye matatizo. Lakini kwa upande wangu ni
ngumu sana kudanganya kwa nafsi yangu kuitangaza huzuni isiyokuwa moyoni
mwangu.
Nakumbuka siku ile aliyonitamkia kwamba hanihitaji tena alisema hakuna
marefu yasiyo na ncha na kwamba amekaa na kutafakari kwa kina na kuona
mimi siendani naye na kwa maana hiyo nitafute msichana mwingine na kama
siwezi basi niwe ‘padre’. Daaaah!!!! iliniuma sana.
Nilisoma ujumbe wake wa kunikataa nikiwa kazini, nafundisha wanafunzi
darasani huku kiu kali ya maji ikiniunguza koo kutokana na uhaba wa maji
katika kijiji nilichopangiwa. Na sio tu kwamba kulikuwa na uhaba wa
maji, mimi pekee ndiye mwalimu niliyekuwa nachagua sana maji ya kunywa,
‘lazima yawe yamechemshwa’ hivyo kuyapata pia ilikuwa mtihani zaidi.
Nilipomaliza kuusoma ujumbe wake, kwakweli nilishindwa kuuhisi ulimi
mdomoni kwangu…mate yalinikauka ghafla. Ilibidi kipindi kiishie
palepale..!
‘Nimeamua kuishi peke yangu, I need to be alone. Naomba uniache, tafuta
mwanamke mwingine, mwalimu mwenzako atakuwa hadhi yako nadhani..!
Ukishindwa unaweza kuwa padre mzuri,” ilisomeka sehemu ya ujumbe wake.
Haya yanaweza kuonekana ni maneno ya kawaida sana…lakini yalitoka kwa
mtu niliyeweza kuwa naye katika mahusiano kwa zaidi ya miaka sita (6) na
nikatumia nguvu kubwa ya kiuchumi kumsaidia katika elimu yake ya Chuo
Kikuu. Baada ya kuhitimu, hii ndo zawadi ya maneno aliyoniandalia kwa
muda wote huo. Kumbe tulikuwa wawili, mimi nikacheza nikijua ndio kila
kitu.
Mwanzoni nilidhani anatania. Lakini kwa jinsi alivyosisitiza nikaanza
kujiuliza kuna jambo gani baya lililomtatiza juu yangu hadi amepata
maneno makali hivyo!! Akili nyingine ilinituma labda kuna mtu kamjaza
habari za uongo juu yangu…lakini katika tafakari na kudadisi nilikuta
hakuna kitu kama hicho.
Hii ilikuwa ni miezi miwili tu tangu ahitimu masomo yake ya Chuo Kikuu
na kwa mipangilio na makubaliano yetu ni kwamba baada ya kuhitimu
tutafanya taratibu za kuishi pamoja katika ndoa. Sikujua nilikuwa naota
ndoto, alinacha kwenye dunia ya Abunuasi.
Hili jambo liliniuma sana na kuanza kujiuliza kipi kipya sana
kimeongezeka kwake hadi kuhisi siendani naye!!! Ni kwanini kwa kipindi
chote hicho asiniambie kwamba hatuendani ili nitafute huyo wa ‘saizi’
yangu? Hadi amesubiri…nimehudumia kwa jasho kubwa na kazi yangu mshahara
kiduchu, amehitimu chuo ndio anasema hivi. It’s so painful!
Haya mambo niliwahi kuyasikia kwenye wimbo mmoja wa zamani sana. Nikajua ni utunzi tu. Mwisho yakanikuta mwenyewe.
Siku tatu baadae, ambayo pia ni siku ya tatu baada ya kumaliza mitihani
yake alinambia hataki tena simu kutoka kwangu wala meseji na kama
nitakuwa na ujumbe basi nimpatie rafiki yake aliyekuwa akiishi naye
hosteli atamfikishia…nilipomuuliza sababu za maamuzi hayo alinijibu kwa
ufupi, “ukija tutaongea”. Na siku aliyokuja baada ya hiyo miezi miwili
aliyokuja nayo ndio hayo.
Siku ya tatu iliwadia, nilijipanga sana kumshawishi ausikie moyo wangu.
Lakini alisisitiza tena kwamba hahitaji nimpigie simu wala kumtumia
meseji kwa sababu hayuko tayari kuwa katika mahusiano na mtu yeyote…na
kweli zilipita siku mbili nikiwa bize kumtafuta katika simu bila majibu.
Nilipoendelea sana, niligeuka kuwa usumbufu kwake.
Itaendelea Kesho....!!!
Utunzi wa Edward Lucas; 0655 545 064
Tags
MY STORY