Kumekuwa na kitendawili juu ya uwezo wa wanyama kuweza kutambua hisia za
binadamu kwa kuwaangalia, huku ikielezwa kuwa ni mbwa pekee ndiye
mnyama ambaye angeweza kutambua hisia kwa mtindo huo.
Lakini hivi karibuni, Wana sayansi wa Chuo Kikuu cha Sussex cha
Uingereza wamefanya utafiti na kubaini kuwa farasi wana uwezo pia wa
kubaini hisia za binadamu aliyekasirika au mwenye furaha kwa kumuangalia
tu.
Wanasayansi hao walitumia picha za wanaume wenye tabasamu na wengine
wenye hasira na kuwaonesha farasi 28 waliochaguliwa kufanyiwa majaribio
na walitoa majibu sahihi.
Amy Smith ambaye alishiriki katika utafiti huo alieleza kuwa farasi
walionesha hali ya uoga walipoona picha ya mwanaume aliyekasirika, na
walitulia walipoona picha ya mwanaume aliye tabasamu.
Ilielezwa kuwa farasi walioneshwa picha ya mtu aliyekasirika
waliiangalia kwa jicho la kushoto zaidi. Sayansi inaonesha kuwa akili za
wanyama zimeumbwa katika hali ambayo hisia zinazotolewa na jicho la
kushoto huangaziwa na eneo la kulia la ubongo ambalo hutumiwa kuangazia
hisia mbaya.
Kadhalika, watafiti hao walieleza kuwa farasi waliooneshwa picha ya mtu
aliyekasirika, mapigo yao ya moyo yalienda mbio zaidi ya pale
walipooneshwa picha ya mwanaume aliyetabasamu.