
Sakata la Serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni
limeibuka upya, safari hii ukielekezwa kwa Rais John Magufuli.
Hata hivyo, shughuli nyingi zinazomshirikisha Rais zimekuwa zikirushwa
moja kwa moja jambo lililomfanya Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Aida
Khenani kuhoji sababu za kuzuia shughuli za Bunge kuonekana moja kwa
moja.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Khenani alisema Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linatumia
kodi za wananchi lakini vikao vya wabunge waliowachagua havionyeshwi
moja kwa moja kuwawezesha kufuatilia wanachozungumza wawakilishi wao.
“Hapo kuna tatizo,” alisema Khemani.
Alihoji kama tatizo ni gharama kama Serikali ilivyoeleza, inakuwaje pale
Rais anapozungumza gharama zinapungua na Bunge linaporushwa moja kwa
moja ndiyo zinakuwa kubwa.
Khenani aliungwa mkono na mbunge mwenzake wa Viti Maalumu (Chadema),
Mariam Msabaha aliyehoji sababu za Bunge kuwa na hofu ya vikao vyake
kuonekana moja kwa moja.
Wabunge hao waliungana na mtangazaji wa zamani wa shirika hilo, Juma
Nkamia (Chemba-CCM) aliyesema mwishoni mwa wiki kuwa shirika hilo
limefika mahali pabaya hadi kuazima mitambo kwa watu binafsi kwa ajili
ya kurusha matangazo ya ziara ya Rais Magufuli mkoani Mtwara.
Nkamia amesema hata studio inayotumika TBC ni ile iliyokuwapo tangu enzi
za TVT na kwamba shirika hilo lina usikivu mbovu wa matangazo na pale
wanaporusha moja kwa moja ni aibu.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura
amesema ni kweli mitambo ya TBC imekuwa chakavu, lakini Serikali
inaifanyia kazi na imeongeza bajeti ya shirika hilo kutoka Sh1 bilioni
hadi Sh3 bilioni.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk
Harrison Mwakyembe alisema hoja ya Bunge Live amekuwa akiijibu na
anachoweza kusema ni kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano
Tanzania (TCRA) imelikabidhi Bunge leseni na sasa litaweza kuamua
lolote.
Pia alijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge kuhusu bajeti ya
wizara yake. Juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii, akisema ni hatari
na isipoangaliwa inaweza kuingiza nchi katika matatizo, hivyo lazima
sheria zichukuliwe dhidi ya wanaokiuka matumizi yake.
Tags
Bungeni