
RAIS John Magufuli Ametoa ombi zito kwa viongozi wa dini nchini wakiwamo
maaskofu baada ya kuwataka wamwombee ili kazi yake ya urais isimpe
kiburi bali aendelee kuwa mtumishi mwema wa watu.
Rais Magufuli alitoa ombi hilo kwa nyakati tofauti jana wakati
aliposhiriki ibada ya Jumapili kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) Usharika wa Moshi Mjini na Kanisa Kuu la Kiaskofu la
Parokia ya Kristo Mfalme (la katoliki), pia la Moshi Mjini, mkoani
Kilimanjaro.
Magufuli aliomba maaskofu na viongozi wengine wa dini wamuombee wakati
akiwa katika kanisa la Usharika wa Moshi, kwenye ibada iliyoongozwa na
Mkuu wa Kanisa la KKKT Tanzania, Askofu Dk. Fedrick Shoo na baadaye
katika Kanisa la Kristo Mfalme ambako ibada iliongozwa na Askofu wa
Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Isaac Amani.
Awali, akiwa katika kanisa la KKKT, Askofu Shoo alimuomba Rais Magufuli
kujitenga na washauri wanaojikomba na badala yake apokee ushauri
unaotolewa na washauri wema na wenye nia njema kwake na kwa taifa.
“Tunamuomba Mungu akupe washauri wazuri wasio na hila na wasiojikomba
kwako….na ambao hawatakuwa na ajenda za kujinufaisha binafsi. Pale
unapoona mambo hayaendi na umepungukiwa, sisi kama kanisa na Watanzania
wenye nia njema tunasema tupo tayari kukushauri na kukuombea,”alisema
Askofu huyo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini.
Aidha, Askofu Shoo alisema pamoja na jitihada mbalimbali za maendeleo
zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya tano, bado kumekuwa na
baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiona mabaya tofauti na yale mazuri
ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali, jambo ambalo sio sahihi.
“Tunamuomba Mungu atupe Watanzania ambao wana uwezo wa kuona mema ambayo
umekuwa ukiyatenda na umekuwa ukiyafanya katika kipindi hiki kifupi
cha utawala wako,” alisema Dk. Shoo
Dk. Shoo aliongeza kuwa kanisa lake litaendelea kuunga mkono jitihada
zinazochukuliwa na serikali katika utumbuaji majipu na kuwashughulikia
wale wote ambao wamekuwa wakiishi kwa kutegemea shughuli za magendo na
rushwa.
Alimwomba pia Rais Magufuli kuangalia uwezekano wa kuzipunguzia taasisi
za dini mzigo wa kodi ambazo wanatozwa pale wanapoingiza mali ambazo
zimekuwa zikitumika kutoa huduma za kijamii.
Wakati alipoitwa na Dk. Shoo ili kutoa salamu kwa waumini wa kanisa
hilo, ndipo Rais Magufuli alipoomba viongozi wa dini wamuombee ili
madaraka aliyo nayo yasimpe kiburi.
Alisema mtu anaweza akapata madaraka na kuwa kiburi, na akafanya mambo
ya ajabu wakati maisha yenyewe ni ya temporary (muda), jambo ambalo yeye
anaomba lisimtokee.
“Mheshimiwa Baba Askofu, ombi lako kuhusu kodi kwa taasisi za dini
nitalibeba na nitalifanyia kazi. Haiwezekani mtu unaagiza X - Ray
machine kwa ajili ya huduma halafu ulipe kodi. Nitazungumza na viongozi
wa Wizara ya Fedha wajadili na kuona namna ya kulishughulikia,”alisema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli alilichangia kanisa hilo (KKKT) mifuko 150 ya saruji kwa
ajili ya shughuli za ujenzi na pia kuizawadia kwaya ya Usharika wa Moshi
Mjini Sh. milioni moja.
IBADA KANISA KRISTO MFALME
Katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Parokia ya Kristo Mfalme, Askofu Amani
alisema ni vyema wananchi wakaendelea kulinda amani na umoja wa taifa
kwani ni dhahiri kuwa amani iliyopo inalindwa pia na wananchi na siyo
majeshi peke yake kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Baada ya kumaliza mahubiri yake, Askofu Amani alimpa nafasi Rais
Magufuli kutoa salamu zake ambapo alisema: “Najua urais mnao ninyi na
mliamua niwe mtumishi wa watu. Naomba muendelee kuniweka kwenye maombi
ili kazi hii ya urais isinipe kiburi… niwe mtumishi wa watu.”
Akieleza zaidi, Rais Magufuli alisema amekuwa mtu wa kufikiriwa vibaya
na baadhi ya watu kwamba ni mtu mkali, lakini ukweli ni kwamba yeye ni
mkali kwa watu wanaofanya maovu.
Alisema ni vyema Watanzania wakaendelea kumuombea ili asiwe na kiburi
cha madaraka na kuendelea kutekeleza kazi aliyopewa na Mungu na kwamba,
amekuwa akifanya mabadiliko makubwa kutokana na ukweli kwamba nchi
ilikuwa inaelekea pabaya.
Rais Magufuli alichangia pia Kanisa la Kristo Mfalme mifuko 100 ya
saruji pamoja na kwaya ya kanisa hilo kiasi cha Sh. milioni moja.
Tags
RAIS MAGUFULI