Aidha, Lissu na wenzake hao wamedhamiria kuona kuwa kigogo huyo
anayetuhumiwa kuliacha jina lake halisi la Daudi Albert Bashite kutokana
na matokeo mabovu ya sekondari na kutumia jina la mtu mwingine,
achukuliwe hatua za kisheria ikiwamo kufungwa jela kwa kosa la kughushi
ikiwa itathibitika kuwa ana hatia.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu ambaye
ni Rais wa TLS, alisema uamuzi huo wa kulifikisha mahakamani suala la
Bashite umetokana na maazimio ya baraza la uongozi la chama hicho, lengo
likiwa ni kulinda utawala wa sheria na uwajibikaji nchini.
Tofauti na matarajio ya baadhi ya watu, sakata hilo la Bashite
halikupatiwa jibu kutokana na ripoti ya uhakiki wa vyeti vya watumishi
wote wa umma iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli Ijumaa kutowagusa
viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wabunge na
madiwani.
Katika kufanikisha nia hiyo ya TLS, Lissu aliyekuwa na viongozi wengine
wa chama hicho wakiwamo Makamu Rais, Godwin Ngwilimi na Wakili Stephen
Kuwayawaya, alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na TLS
kufungua mashtaka binafsi ya jinai dhidi ya mkuu huyo anayedaiwa kuitwa
Bashite.
Aliongeza kuwa mkuu huyo wa mkoa, anatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya
jinai likiwamo hilo la kutumia vyeti feki na kwamba, kazi ya kumshtaki
haitachukua miezi bali ni wiki mbili au tatu.
“Kifungu cha 128(2) cha sheria ya Mwenendo wa jinai, sura ya 20 ya
sheria za Tanzania kinaruhusu mtu binafsi (pamoja na taasisi, kampuni au
mashirika kama TLS) kupeleka malalamiko kwa hakimu mwenye mamlaka pale
anapoamini kuna sababu za msingi zinazoonyesha kuwa kosa la jinai
limetendwa,”alisema Lissu, akielezea vifungu wanavyotumia kufikisha
suala hilo kortini.
Alisema dhana ya utawala wa sheria ina maana pana na kwamba, pamoja na
mambo mengine, siyo tu kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria, bali pia
kila mtu bila kujali cheo au nasaba na hali yake kiuchumi na jamii,
yuko chini ya udhibiti wa sheria za kawaida za nchi na hivyo yuko pia
chini ya mamlaka ya mahakama za kawaida.
“Kuna tuhuma za muda mrefu sasa kwamba Mkuu huyo wa mkoa ametumia vyeti
vya shule ya sekondari visivyokuwa vyake. Yeye… ni Daudi (Albert)
Bashite,” alisema Lissu, akiongeza kuwa jina linalotumiwa sasa na mkuu
huyo linadaiwa kuwa mwenyewe yupo na ndiye mwenye vyeti halisi, na
kitendo hicho ni kosa la jinai.
Akifafanua zaidi, Lissu alisema kifungu cha 120 cha Kanuni ya Adhabu,
Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, kinasema “Mtu yeyote aliye kwenye
utumishi wa umma ambaye, wakati akitekeleza majukumu ya ofisi yake
akifanya kitendo cha udanganyifu au ukiukaji dhamana hiyo ungekuwa ni
kosa la jinai kama ungefanywa na mtu binafsi au la, anafanya kosa na
endapo atapatikana na hatia atapata adhabu ya kifungo cha miaka saba
jela.”
Lissu alisema kwa kutumia vyeti vya shule visivyokuwa vyake, na kwa
kutumia majina ya mtu mwingine wakati akiwa mtumishi wa umma, mkuu huyo
mwenye jina halisi la Daudi Bashite ameathiri imani ya wananchi kwa
serikali yao kwa kuajiri na kulinda watu wadanganyifu na wasiokuwa na
vyeti halali.
“Mtu huyu amefanya kosa la jinai ambalo kwalo anastahili kushtakiwa
mahakamani na endapo atapatikana na hatia anastahili kuadhibiwa kwa
mujibu wa sheria za kawaida za nchi yetu,” alisema Lissu ambaye pia ni
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema).
Lissu aliongeza kuwa endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atakataa kutoa
ridhaa, TLS itamfungulia mkuu huyo wa mkoa mashataka ya rejea ya
kimahakama katika Mahakama Kuu ili alazimishwe kutoa ridhaa hiyo.
Kabla ya kumkabidhi Rais Magufuli ripoti ya uhakiki wa vyeti vya elimu
na kitaluma kwa watumishi wa umma nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Utumishi na Uatawala Bora, Angela Kairuki, alisema watumishi 9,932
walikutwa na vyeti vya kughushi na kwamba, ripoti hiyo haikuwagusa
viongozi wa kisiasa wakiwamo mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,
wabunge na madiuwani.
Hata hivyo, Makamu Rais wa TLS, Ngwilimi, alisema kuwa kwa mujibu wa
kifungu cha Sheria ya Utumishi wa Umma namba 3 na 5, tafsiri ya mtumishi
wa umma inawahusisha pia Wakuu wa mikoa na Wakuu wa Wilaya na hivyo
kina Bashite walipaswa pia kuhusishwa katika uhakiki huo.
