
Bunge la Afrika Mashariki (Eala) lililoanza kikao chake cha siku 14
jijini hapa na cha mwisho kwa Bunge la Tatu linalofikia ukomo Juni 4
limelitaka Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki kuharakisha uchambuzi
wa kikosi kazi kilichoundwa kuchunguza ufisadi katika Sekretariati ya
EAC.
Baada ya dua jana (Jumanne), Abubakar Ogle alisimama kwa kutumia kanuni
za Bunge ibara ya 30 (l) inayompa mbunge uwezo wa kuwasilisha hoja
mahsusi yenye masilahi kwa umma na kwa haraka, na baada ya kupewa nafasi
alitaka Bunge lijadili mustakabali wa EAC baada ya taarifa ya uchunguzi
kubaini ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Amesema kikosi kazi kilichoundwa licha ya kujiridhisha na tuhuma
zilizojitokeza kulingana na taarifa ya mtumishi wa EAC aliyemaliza muda
aliyedai kuna ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za jumuiya, pia
kilibaini mambo zaidi ya yaliyotarajiwa ambayo yanafanya uhai wa EAC
kuwa shakani.
Spika wa Bunge la Eala, Daniel Kidega alimtaka mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri wa Afrika Mashariki ambaye ni Naibu Waziri wa Afrika Mashariki
wa Uganda, Julius Maganda kujibu hoja hiyo.
Maganda amesema uchunguzi umekamilika ila bado haujawasilishwa kwenye baraza.
"Mheshimiwa Spika naliomba Bunge liwe na subira, tutakapokuwa tumepata
taarifa kamili ya uchunguzi tutaifanyia kazi kwa kutoa mapendekezo kwa
wakuu wa nchi za EAC," amesema Maganda
Wabunge walichangia hoja hiyo ni Bernard Mulengani, Dora Byamkama, Sarah
Bonaya, Agnes Mumbi na Nancy Abisai, ambaye alionyesha hofu juu ya
mustakabali wa jumuiya katika mazingira yanayoendelea katika
Sekretariati ya EAC.
Patricia Hajabakiga, amesema vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya
ofisi haviwezi kukubalika na jukumu la Bunge ni kusimamia mihimili
mingine ili kuhakikisha utawala bora unakuwapo.