Mkuu wa Shule
ya St. Joseph Cathedral, Sista Theodora Faustine akimkabidhi zawadi na
cheti, Prof. Rwekaza Mukandala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye
mahafali ya sita ya kidato cha sita, ili ampatie mhitimu. Mahafali hayo
yalifanyika Jumamosi, Mei 13, 2017 shuleni hapo. (Picha na Irene Bwire)
Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Rwekaza Mukandala ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya sita ya kidato cha sita ya Shule
ya St. Joseph Cathedral, akizungumza na wahitimu (hawapo pichani).
Mahafali hayo yalifanyika Jumamosi, Mei 13, 2017 shuleni hapo. (Picha na Irene Bwire)
Viranja wa
darasa la PCM, Martin na Nsobya Musona wakipokea zawadi ya keki kutoka
kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. Rwekaza
Mukandala ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya sita ya kidato
cha sita ya Shule ya St. Joseph Cathedral, yaliyofanyika Jumamosi, Mei
13,2017) shuleni hapo. (Picha na Irene Bwire)
Baadhi ya wazazi, walezi na ndugu
walioshiriki mahafali ya sita ya kidato cha sita ya shule ya sekondari
ya St. Joseph Cathedral yaliyofanyika Jumamosi, Mei 13, 2017 shuleni
hapo.
(Picha na Irene Bwire)
Mwenyekiti wa
Bodi ya shule, Bibi Margreth Ikongo akitoa shukkrani mgeni rasmi, Prof.
Rwekaza Mukandala pamoja na wazazi na walezi walioshiriki mahafali ya
sita ya kidato cha sita ya shule ya sekondari ya St. Joseph Cathedral
yaliyofanyika Jumamosi, Mei 13, 2017 shuleni hapo. (Picha na Irene Bwire)
………………………………………………………………………..
*Asema utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa fedha
MAKAMU MKUU wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Prof. Rwekaza Mukandala amewataka vijana wanaohitimu
kidato cha sita nchini wawe makini na wasikubali kusombwa na mawimbi ya
dunia.
Ametoa wito huo jana (Jumamosi,
Mei 14, 2017) wakati akizungumza na wahitimu 237 wa kidato cha sita wa
shule ya sekondari ya St. Joseph Cathedral kwenye mahafali ya sita ya
shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, jijini Dar es Salaam.
Prof. Mukandala alisema: “Kwa
hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake
kimaisha. Kuweni makini, msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta
mmepoteza ndoto zenu,” alisisitiza.
“Kuhitimu kidato cha sita si
jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongiza kujiandaa na utu uzima ikiwemo
kujiunga na elimu ya vyuo vya juu na kuingia kwenye ndoa. Ni muda wa
kutathmini yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni
fursa ya kutoa shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya
kazi kwa umakini na kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa,”
alisema.
Alisema kuanzia sasa kila mmoja
wao anapaswa kujiamini, kujituma zaidi na kujiona kuwa ana wajibu wa
kujiletea maendeleo binafsi. “Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona
mnyonge, au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa
makini na maisha yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,”
alisisitiza.
Aliwataka wahakikishe
wanakuchukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma
wanazozitaka. Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote
lakini pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na
kujilimbikizia mali.
“Epukeni rushwa na ufisadi.
Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa
fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa
kuzingatia mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.
Akitoa mfano, Prof. Mukandala
alisema: “Msikimbilie kuwa na magari mengi bila kujua nani atayatumia,
au kujenga nyumba kubwa bila kujua nani atahitaji nafasi hiyo kubwa.
Unanunua simu mbili au tatu bila kufikia athari zake kwa afya na
mahusiano yako. Kabla hujachukua hatua ni lazima ujiulize, je
unakihitaji kitu hicho? Kuweni makini na matumizi ya fedha badala
kujilimbikiza vitu vya anasa,” alisema.
Aliwataka wazazi waendelee
kuwalea vema vijana hao kwa sababu bado wanahitaji usimamizi wa wazazi
kwa kila hatua wanayosonga mbele. “Tuendelee kuwaunga mkono watoto wetu
kwa sababu jukumu letu kama wazazi bado liko palepale,” alisema.
Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi
kuzungumza na hadhira iliyokuwepo, Mkuu wa Shule ya St. Joseph
Cathedral, Sista Theodora Faustine alisema St. wanafunzi waliohitimu
jana ni 237 ambao kati yao wavulana ni 140 na wasichana ni 97 waliokuwa
wakichukua michepuo ya ECA, EGM, CBG, HGE, HGL, PCM, PCB na PGM.
Alisema anaamini kwamba wahitimu
wote watakuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu kwa sababu
shule hiyo imekuwa ni ya kwanza yenye wingi wa ufaulu kuliko shule
yoyote mkoani Dar es Salaam. “Tumekuwa tukipata wanafunzi bora kitaifa
mara kwa mara na mwaka jana tulipata wanafunzi bora kutoka michepuo ya
PCB na ECA,” alisema.
Sista Theodora alisema wamekuwa
wakifaulisha wanafunzi zaidi ya 250 kwa mwaka na kwa maana hiyo,
wameweza kuandaa vijana 250 kuingia kwenye vyuo vikuu vya ndani na nje
ya nchi. Akifafanua kuhusu malengo ya shule, Mkuu huyo wa shule alisema
lengo lao ni kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania na kuwandaa kuwa
wawajibikaji kwa Mungu na kwa Taifa lao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa
wazazi wenye watoto waliohitimu kwenye mahafali hayo, bw. Eric Shigongo
alisema kila mhitimu anayo ndoto yake ambayo anapaswa kufanya kila
awezalo kuhakikisha ndoto yake inatimia.
“Unao uwezo wa kuchagua (power of
choice) kilicho chema kwa ajili ya maisha yako ya baadaye. Nasisitiza
kwa sababu najua kila mmoja wenu ana ndoto yake ya kufika mahali fulani.
Hakikisha unatimiza ndoto hiyo, haijalishi utapitia mazingira gani,”
alisema.
Alisema kwake yeye anawaona
vijana waliohitimu kwamba ni washindi (champions) na aliwaeleza hivyo
wiki tatu kabla ya kuanza mitihani yao. Hata hivyo, aliwaasa kwamba wawe
tayari kukosa mambo mengine kama kweli wanataka kufanikiwa maishani
mwao.
“kama unataka kufanikiwa
maishani, huna budi kujinyima mambo mengi ili uweze kupata kile
unachokitaka. Najua mmemaliza kidato cha sita lakini safari yenu ya
maisha ndiyo kwanza imeanza. Ninaamini wako watu hapa watakaotusaidia
kutatua changamoto za nchi hii, wako madaktari hapa, wako wahandisi,
wako wafanyabiashara na yuko Rais ajaye wa Tanzania, tena Rais mwanamke
kutoka katika kundi hili,” alisema.
Katika mahafali hayo, mwanafunzi
Kauthar Said aliibuka mwanafunzi bora na kupewa zawadi ya kompyuta
mpakato (laptop) na wanafunzi wa mchepuo wa PCM, walipewa zawadi ya keki
na Mkuu wa Shule kwa kuwa ni darasa ambalo halijawahi kuwa na kesi
yoyote ya utovu wa nidhamu katika kipindi cha miaka miwili waliyoakaa
shuleni hapo.
Tags
VIJANA