Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” na kushoto ni Kaimu Naibu
Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Nd. Abdulghafar Idrissa akifanya kazi ya
kukandika udongo katika nyumba ya mwananchi Bi. Asha Abdalla wa Shehia
ya Fuoni Migombani aliyebomokewa nyumba yake kutokana na maafa ya mvua
zilizonyesha juzi Unguja.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika harakati za ujenzi wa nyumba hiyo uko Fuoni Migombani Unguja.
Baadhi ya wananchi wakiwa katika harakati za ujenzi wa nyumba hiyo uko Fuoni Migombani Unguja.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” akitoa shukrani zake kwa
wananchi mbali mbali walioshiriki katika ujenzi huo na kuhakikisha
Bi.Asha Abdalla anapata makaazi ya kuishi. Picha na Afisi Kuu CCM
Zanzibar.
………………………………………………………
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WANANCHI visiwani vya Zanzibar
wameshauriwa kuendeleza kwa vitendo Utamaduni wa uzalendo wa
kusaidiana wakati wa maafa mbali mbali yanayotokea nchini bila kujadili
tofauti za kisiasa na kidini.
Wito huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” mara
baada ya ujenzi wa nyumba ya Balozi wa Nyumba kumi Bi. Asha Abdalla
Baruti iliyobomoka kutokana na maafa ya mvua zinazonyesha nchini, huko
Fuoni Migombani.
Dkt. Mabodi alisema maafa
yanapotokea hayachagui sehemu ya kuathiri bali yanawakumba wananchi wote
hivyo ni muhimu wanajamii kushirikiana kwa mambo ya kijamii na
kimaendeleo na kuacha siasa za utengano na chuki.
Ujenzi huo umefanyika kutokana na
agizo la Naibu Katibu Mkuu huyo alipowataka uongozi wa CCM na UVCCM
Wilaya ya Dimani Unguja, kumjengea makaazi ya muda mwananchi huyo ambaye
hakuwa na sehemu ya kuishi kutokana na nyumba yake kuharibiwa na mvua
zilizonyesha hivi karibuni.
Alisema hatua ya Chama hicho
kutoa msaada na kushiriki katika masuala ya shughuli za kijamii kwa
wananchi itakuwa ni utamaduni endelevu kwa Unguja na Pemba.
Alieleza kwamba lengo la CCM
kutoa msaada wa kujenga makaazi ya dharura kwa wananchi wakati wa
kipindi hichi cha maafa ni kuendeleza kwa vitendo siasa za waasisi wa
vyama vya ASP na TANU ambao walishiriki katika masuala mbali mbali ya
kitaifa na kimataifa kwa lengo la kuwa karibu na wananchi waliowapa
ridhaa ya uongozi.
Pia alisema wakati wa Kampeni za
Uchaguzi CCM ilikuwa ikienda kwa wananchi katika maeneo mbali mbali
kuomba kura za kuiweka madarakani hivyo hata kwa kipindi cha maafa na
changamoto zinazoikabili jamii ni lazima kirudi kwa wananchi kuwaunga
mkono na kuwafariji kwa vitendo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema
CCM ya sasa Viongozi wa ngazi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali
kurudi kwa wananchi kujua changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi
kwa wakati ni jambo la lazima na sio la hiari.
“ Nasaha zangu kwa wananchi ni
kwamba pindi yakitokea maafa hasa magfuriko tusaidiane kwanza kupitia
umoja wetu katika mitaa mbali mbali tunayoishi kwa kuwahifadhi katika
maeneo salama wenzetu wanaopata maafa huku tukisubiri serikali zetu
zichukue hatua za kutoa misaada.”, alisema Dkt. Mabodi.
Pamoja na hayo aliwataka vijana
nchini kuwa mstari wa mbele kwa kujitokeza muda wowote kusaidia masuala
ya ujenzi wa miundombinu iliyoharibiwa na maafa ili nchi iweze kujivunia
uwepo wa kundi hilo ambalo ndio nguvu kazi ya taifa.
Pia aliwataka viongozi wa kisiasa
nchini kuondokana na mazoea ya kulalamika na kulaumu serikali hasa
katika kipindi hichi cha maafa na badala yake wawe sehemu ya
kuwahamasisha wafuasi wao wajitolee kuwasaidia watu waliofikwa na maafa
huku serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kutatua tatizo
hilo.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la
Fuoni, Mh. Yussuf Hassan Iddi amesema jimbo hilo litaendelea kusaidia
awamu kwa awamu wananchi mbali mbali waliopata maafa ili waweze kurudi
katika hali yao ya kawaida.
Alisema uongozi wa jimbo hilo
baadae utahakikisha unajenga nyumba ya kudumu kwa mwananchi huyo ili
aweze kupata uhakika wa makaazi yake.
Kwa upande wake Mbunge Mteule wa Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM , Dkt.Abdulla Hasnuu
Makame alisifu hatua zilizochukuliwa na CCM kwa kuendeleza utaratibu wa
kuwafariji wananchi wakati wa matatizo mbali mbali ya kitaifa .
Aliahidi kuiwakilisha vyema CCM
katika Bunge hilo ili fursa mbali mbali zinazopatikana ziweze kusaidia
katika kuimarisha miradi ya kijamii hasa kuongeza miundombinu ya
barabara, Elimu, Afya na ajira kwa vijana.
Mapema Bi. Asha Abdalla
ameishukru CCM na wananchi wote walioshiriki katika zoezi la kumjengea
nyumba yake na kuongeza kwamba hatua hiyo imemfariji na kumpa nguvu za
kuendelea kufanya kazi za kujipatia kipato kwa ufanisi zaidi.
Tags
VIONGOZI WA CCM