
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
jana tarehe 16 Mei, 2017 amefanya ziara katika ofisi za Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo amekagua miundombinu ya shirika hilo na
kuzungumza na wafanyakazi.
Mhe. Rais Magufuli amejionea jinsi miundombinu ya shirika hilo
inavyokabiliwa na changamoto mbalimbali za uchakavu na teknolojia duni
na amesema Serikali itafanyia kazi changamoto hizo ikiwa ni pamoja na
kujenga majengo mapya ya studio za kisasa za kurushia matangazo katika
makao makuu ya nchi Mjini Dodoma.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ambaye hivi karibuni ametoa Shilingi
Bilioni 3 kwa ajili ya kuisaidia TBC amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa shirika
hilo Dkt. Ayub Rioba kutumia fedha hizo kutatua matatizo ya uhaba na
uchakavu wa vifaa vya uzalishaji wa vipindi na urushaji wa matangazo,
kununua vyombo vya usafiri na kufanya ukarabati wa majengo.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi amewahakikishia kuwa Serikali itaboresha
stahili zao kwa mujibu wa utaratibu uliopo na papohapo amemuagiza Dkt.
Rioba kulipa mara moja malimbikizo ya posho zote ambazo wafanyakazi hao
wanadai kuanzia Mwezi Oktoba 2016, zilizofikia shilingi Bilioni 1 na
milioni 285.
Mhe. Rais Magufuli ametaka wafanyakazi wa TBC kufanya kazi kwa juhudi,
maarifa na ubunifu wa hali ya juu ili matangazo ya chombo hicho cha
Taifa yawavutie Watanzania wengi, na kiwe chombo kinachoongoza nchini.
“Msemaji wa Serikali mkubwa ni TBC1 na Redio ya Taifa, nyinyi hamuwezi
mkawa kama vyombo vingine ambavyo vina malengo yao ya kufanya biashara,
nyinyi kazi yenu ni kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania bila kubagua
vyama vyao, bila kubagua dini zao, bila kubagua makabila yao, huo ndio
uwe msimamo mkuu.
“Mmetoa mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, hilo ni lazima niseme,
hata vipindi vyenu ukiviangalia ni vizuri vinaeleza mpaka maisha ya
vijijini, na mimi ni shabiki mkubwa sana wa TBC, lakini tatizo lenu
mnashindwa kwenda na wakati wa sasa” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe aliyekuwepo katika ziara hiyo
kuuangalia Mkataba kati ya TBC na Star Times na kuchukua hatua
zinazostahili endapo itabainika kuwa mkataba huo hauna manufaa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
16 Mei, 2017