
RAIS Dk. John Magufuli amesema serikali itawachuguza na kuwachukulia
hatua baadhi ya wafanyakazi ambao wamebadili umri wao ili waendelee
kuwepo kwenye ajira serikalini.
Akizungumza jana kwenye sherehe ya sikukuu ya wafanyakazi dunia
zilizofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi
mkoani Kilimanajaro, alisema wapo wafanyakazi ambao wamebadilisha umri
wao na wanaendelea kuwepo kwenye ajira licha ya kwamba wamezeeka na
walistahili kustaafu.
“Wapo watumishi ambao wamebadilishi umri wao wa kuishi wamebadilisha
miaka yao, unakuta ni mzee kabisa lakini yeye hastaafu tu huyo naye hana
utofauti sana na mfanyakazi hewa, kwa sababu ameshamaliza muda wake
hataki kutoka kazini awaachie wengine nao wafanye kazi anaendelea kukaa
pale kubadilisha miaka,”alisema.
“Mimi hapa nilipo nilikuwa nimebakiza miaka miwili tu kustaafu lakini
hebu kaangalieni kwenye maofisi yenu wapo watu ambao ni wazee kuliko
mimi bado wanafanya kazi na wanasema ndio wakati umefika, hawa nao dawa
yao tunaichunguza” Rais Magufuli alisema kimsingi kazi ya kuondoa
wafanyakazi hewa imeenda vizuri na limefikia asilimia 98 lakini bado
halijaisha.
Aliongeza kuwa katika fedha tu za watumishi hewa, ukichukulia tu
mshahara serikali ilikuwa inapoteza Sh. bilioni 19.8 kwa mwezi na kwa
mwaka ni zaidia Sh. Bilioni 230.