
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ameeleza kusikitishwa na taarifa za kifo cha Mbunge mstaafu wa Jimbo la
Moshi mjini Mzee Philemon Ndesamburo kilichotokea asubuhi ya leo.
Katika salamu za rambirambi alizozitoa Rais Magufuli kwenda kwa wafiwa
pamoja na viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) amesema amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
“Kwa masikitiko nimepokea taarifa za kifo cha Mbunge Mstaafu wa Jimbo la
Moshi Mjini, Mzee wangu Philemon Ndesamburo kilichotokea leo tarehe 31
Mei, 2017 katika hospitali ya rufaa ya KCMC iliyoko Moshi Mkoani
Kilimanjaro. Namkumbuka Mzee Ndesamburo kwa hekima zake na uongozi wake
uliozingatia siasa za kistaarabu” alisema Rais Magufuli
Aidha, Rais Magufuli amesema alifanya kazi na marehemu Philemon
Ndesamburo wakati wote wakiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na wakati wote walishirikiana, kutaniana huku akimkumbuka kwa
namna ambavyo alitumia muda wake bungeni kupigania mambo yenye maslahi
kwa wananchi wa jimbo lake la Moshi Mjini.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameitaka familia ya marehemu Philemon
Ndesamburo na wote waliguswa na msiba huo kuwa na moyo wa subira,
uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu walichonacho.
Kwa upande mwingine Rais Mgufuli amemuombea dua marehemu apumzishwe mahali pepa peponi
Tags
RAIS MAGUFULI