
Bunge jana lilielezwa kuwa msanii aliyebuni na kutengeneza nembo ya
taifa ya Bibi na Bwana, Francis Ngosha ametelekezwa na taifa na anaishi
maisha magumu.
Suala la msanii huyo liliibuka Bungeni mjini Dodoma leo, kutokana na
mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Temeke (CUF), Abdalah Mtolea, ambaye
amesema msanii huyo hajanufaika na ubunifu wake huo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga kilele hapa tukidai haki miliki ya
wasanii wetu ili kazi zao ziweze kuwanufaisha wao na familia
zao,”amesema Mbunge huyo akiegeme kanuni ya 68(7) na 47(1).
“Kumekuwa na kilio na malalamiko makubwa ya Bwana Francis Ngosha ambaye
ndiye aliyebuni ngao (nembo) ya taifa ambayo tunaitumia kwa kiasi
kikubwa na tunajivunia ngao hii,”amesema.
“Lakini mtu huyu hajawahi kunufaika kwa kazi hii ya mikono yake anaishi
pale Buruguni maisha ya ajabu maisha mabovu, afya yake ni mbaya na
anashindwa hata kwenda kupata tiba,”amesisitiza.
“Anaishi kwa shida wakati ngao yake inaheshimika hata hapa kwenye jengo
letu. Hivi kweli na sisi kama Bunge tunaingia kwenye dhambi hii ya kula
jasho la mtu ambalo hajalipwa haki yake?”amehoji.
Akijibu muongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Mussa Zungu, alisema
kwa maoni yake haoni sababu ya shughuli za bunge kuahirishwa ili
kujadili suala hilo bali Serikali ilitolee maelezo.
“Hili la kwako halina udharura litajibiwa na waziri wa nchi (Jenister
Mhagama). Inawezekana Serikali ina majibu yake ama mmemsaidia lakini
zile pesa zikaenda zikapigwa na watu pembeni,”amesema.
Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia
Sera,Bunge,Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, alisema Serikali italichukua
suala hilo kuona njia bora ya kulishughulikia.
“Serikali inampongeza sana msanii huyu kwa kuweza kufanikisha nchi yetu
kuwa na nembo tunayojivunia wote. Sisi kama Serikali tunapaswa
kuichukua,”amesema Mhagama na kuongeza;-.
“Tutakwenda kuangalia namna hoja hii itaweza kupewa uzito. Kwa ujumla
naomba niseme msanii amefanya kazi kubwa sana na taifa letu limeendelea
kutambulika kwa kutumia kazi hiyo,”amesema.
Tags
nembo ya taifa