
SHEKHE Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salim, amewaomba
wafanyabiashara wasipandishe bei ya bidhaa katika kipindi cha Mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Alitoa maombi hayo jana kutokana na alichosema ni tabia ya baadhi ya
wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa zao wakati wa Mfungo huo ili
kujinufaisha binafsi.
“Vyakula vinapanda katika kipindi cha Mfungo na kuwasababishia baadhi ya
wafungaji kutomudu hali hiyo, vitu vinakuwa na bei kubwa kuliko miezi
ya kawaida,” alisema Salim.
Alisema ni vema Waislamu kujianda katika kipindi cha kuikaribisha
Ramadhan kwa kutenda yaliyo mema na kuacha mabaya yasiyompendeza Mungu.
“Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni wa kila Mwislamu, kila mmoja anatakiwa
kutii kwa kufunga na wala si jambo la hiyari ni lazima, kwa kila mwumini
mwenye uwezo na vigezo vya kufunga,” alisema Alhad.
Aliwataka Waislamu kuwasaidia wasiojiweza kama kukaa na yatima na
kuwalisha vyakula akisema hali hiyo itawajengea misingi bora katika
kumsaidia asiye na kitu.
Katika hatua nyingine, aliwataka Waislamu kuliombea amani Taifa na watu
wa mkoa wa Pwani waliokabiliwa na matukio ya mauaji ya kutumia silaha
akisema:
“Nawaomba Waislamu tuiombee nchi yetu ya Tanzania amani hasa wenzetu wa
mkoa wa Pwani kwa majanga yaliyotokea na tuombee vyombo vyetu vya ulinzi
kuimarika ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu.”
Tags
mfungo wa ramadhani