Na: Frank Shija – MAELEZO
WADAU mbalimbali wameipongeza
Serikali kwa uamuzi wa kuivunja Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu
Dodoma (CDA) iliyofikiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Wakitoa maoni yao juu ya umauzi
huo wa Serikali, wameeleza kuwa kuvunjwa kwa Mamlaka hiyo kumekuja
wakati muafaka kwani kutapunguza kero na migogoro ya ardhi iliyokuwa
ikiendelea katika Manispaa ya Dodoma.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Maalum iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jordan Rugimbana,iliyokuwa
inashughulikia changamoto za wananchi dhidi ya CDA, Bw. Aron Kinunda
alisema kuwa uamuzi huo huko sahihi kwani umekuja wakati muafaka kwa
kuzingatia malengo halisi ya uanzishaji wa mamlaka hiyo kuwa
yamekamilika kwa asilimia kubwa ukizingatia na mahitaji halisi ya wakati
huu.
“Ni hatua nzuri katika mustakabari
wa maendeleo ya Dodoma, kwani sasa migogoro mingi ya ardhi iliyokuwa
inatokana na mgongano wa kisheria haitarajiw kujitokeza tena na badala
yake Manispaa itajikita katika kuweka mazingira rafiki ya umiliki wa
ardhi ikiwemo kuongeza muda wa hati ya umiliki kutoka miaka 33 hadi 99
kama ambavyo maeneo mengine ya nchi yanavyofanya.” Alisema Kinunda.
Aliongeza kuwa wananchi watakuwa
wamefarijika sana kwani walikuwa wanaiona CDA kama adui yao mkubwa
ambapo imesababisha malalamiko mengi ya kuchukuliwa ardhi zao bila ya
kulipwa fidia na urasimu katika upimaji na utoaji wa hati za viwanja.
Kumekuwa na malalamiko ya muda
mrefu kutoka kwa wananchi kuwa CDA hakuna usimamizi mzuri wa ardhi jambo
linalosababisha kuwepo kwa migogoro mingi ya ardhi itokanayo na
mgongano wa kisheria uliopo kati ya Mamlaka hiyo na Manispaa ya Dodoma.
“Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya
mwaka 1999 inatambua umiliki wa ardhi upo chini ya Serikali za Mitaa,
kitu ambacho kwa Dodoma ni tofauti kwa kuwa ardhi yote iliyopimwa iko
chini ya CDA kitu ambacho hata Manispaa imekuwa mpangaji,” aliongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoani Dodoma, Mzee Chidawali amesema kuwa
uamuzi wa uamuzi huo umepokelea kwa nderemo na vifijo na ambapo asilimia
kubwa ya wakazi wa Dodoma wanaona ni kama ukombozi kwao.
“ Rais Magufuli anapaswa
kupongezwa sana kwa uamuzi aliouchukua wa kuivunja CDA hakika amefanya
jambo jema sana, sasa wananchi watapata ahueni katika kushughulikia
masuala yao ya umiliki wa ardhi,” alisema Chidawali.
Aidha aliongeza kuwa katika upande
wa taaluma ya uandishi wa habari uamuzi huo umewasaidia kurejesha
uhusiano mwema baina yao na wananchi kwani wamekuwa wakiacha kuripoti
habari za maendeleo badala yake wamekuwa wakijikuta wanaandika habari
kuhusu migogoro ya ardhi zaidi iliyokuwa inasababishwa na CDA.
Chidawali alisema kuwa baada ya
kupata taarifa juu ya uamuzi huo amepata fursa ya kusikia maoni ya wadau
mbalimbali ambapo kwa nyakati tofauti wamempongeza Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuchukua hatua jambo linalotoa tafsiri chanya juu ya
dhamira njema ya Serikali yake ya kuwajali wanyonge.
“Binafsi nje ya taaluma ya habari
mimi ni mzawa wa Dodoma tumekuwa na malalamiko ya muda mrefu hasa kuhusu
uhalali wa kumiliki ardhi, tunaitwa wavamizi katika maeneo ambayo
tumekuwa tukiyamiliki enzi na enzi,” alifafanua Chidawali.
Naye Mwenyekiti wa Soko la Chadulu
Jakton K. Matoto amesema kuwa Jumuiya yao imepokea kwa mikono miwili
uamuzi huo na kuongeza kuwa ni imani yao kuwa baada ya Manispaaa
kuchukua majukumu ya CDA itakwenda kufanya mapitio na kutatua migogoro
yote iliyokuwa ikiendelea kutokana na uwepo wa mamlaka hiyo.
Mwenyekiti huyo ameonyesha
matumaini ya mji wa Dodoma kukua kutokana na kile anachodai kuwa CDA
ndiyo cahnzo cha Dodoma kubaki nyuma kimaendeleo kwani wawekezaji wengi
wamekuwa wakishindwa kuwekeza kutokana na muda mfupi wa hati ya umiliki
wa ardhi ambapo mmiliki anapewa miaka 33 wakati maeneo mengine ya nchi
muda ni miaka 99.
Wakati huohuo Matoto ametoa rai
kwa Manispaa ya Dodoma kujipanga ili kuendana na hali ya mahitaji ya
sasa ikiwa ni mapoja na upimaji wa viwanja kwa kuzingatia misingi ya
haki na usawa.
Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao
Makuu Dodoma ilianzishwa mwaka 1973 kwa malengo ya kutengeneza master
plan na kufanikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo zaidi ya
ekari 260,000 za ardhi zimepimwa na na kupatiwa hati zinazomilikiwa na
CDA, kufuatia kuvunjwa kwake na maelekezo ya Rais kuwa rasirimali zote
ziwe chini ya Manispaa ya Dodoma ambayo itaendeleza shughuli zilizokuwa
zikifanya na mamlaka hiyo kwa mujibu mtaratibu na sheria za nchi.
Tags
MAGUFULI AIFUTA CDA