Jovina Bujulu- Maelezo
Hivi karibuni, Tanzania
ilitembelewa na ugeni wafanyabiashara zaidi ya 80 kutoka Afrika Kusini
ambao uliongozwa na Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kwa lengo la
kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Ujio huo ulikuwa na nia ya kusaini makubaliano katika nyanja za biashara na uwekezaji, Bioanuwai na utalii na uchukuzi.
Makubaliano hayo ambayo
yamegawanyika katika sekta za elimu, mifugo, kilimo, madini, afya,
sayansi na teknolojia na ulinzi na usalama ni kelelezo tosha kuonyesha
dhamira ya mshikamano wa nchi hizi mbili katika kujiletea maendeleo
kiuchumi na kijamii.
Katika eneo la sekta ya elimu
ushirikiano huo utahusisha utafiti, kubadilishana uzoefu wa walimu,
ambapo Serikali hizi zimeingia makubaliano yanayotoa fursa nzuri kwa
Watanzania kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili katika taasisi za
elimu zikiwemo shule na vyuo vikuu nchini humo.
Ugeni wa Rais Zuma na ujumbe wake
nchini umeleta neema kwa Watanzania kwani watapata fursa nyingine ya
ajira nje ya nchi ambapo pia watapata fursa ya kupata uelewa mpana wa
mambo mbalimbali nchini Afrika Kusini na pia kuitangaza nchi yetu katika
nyanja kimataifa.
Akizungumzia fursa hiyo, Rais
Magufuli alisema kuwa walimu hao watapelekwa nchini humo wakati wowote.
Hatua hiyo inatoa fursa nyingine kwa walimu wa Kiswahili na wataalamu
wabobezi wa lugha hii kujipatia ajira na pia kupata fursa ya kuitangaza
lugha ya Kiswahili kimataifa.
Fursa hii ni muhimu, hivyo ni vema
walimu wa Kiswahili na wataalamu waliobobea katika lugha hii
wakaichangamkia ikizingatiwa hapa nchini ndiyo lugha ya Taifa na lugha
inayotuunganisha ambayo pia ilitumika katika kurahisisha harakati za
ukombozi wa nchi yetu.
Katika kuonyesha nia ya dhati ya
kukuza lugha hii, hivi karibuni Rais Dkt. John Magufuli aliahidi
kupeleka walimu wa lugha ya Kiswahili nchini Ethiopia na Rwanda. Aidha,
Rais amekuwa mfano mzuri kwa kutumia lugha hii katika shughuli za
Serikali akiwa hapa nchini au hata nje ya nchi.
Ndio maana mara kwa mara amekuwa
akisisitiza kwa kusema anakipigia debe Kiswahili ili kiweze kuendelea
kutumika katika nchi mbalimbali duniani.
Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa
lugha zinazotumiwa na watu wengi duniani. Kwa sasa inakisiwa kuwa
watumiaji wa lugha hii duniani wapatao zaidi ya milioni 120.
Wito kwa Watanzania wenye sifa,
kuchangamkia fursa nyingine ya ajira ambayo sio tu itaipaisha lugha ya
Kiswahili bali pia itawape heshima walimu watakaokwenda kufundisha
nchini humo.
Aidha, kwa watakaofanikiwa kwenda
huko wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu kwa kutangaza mazuri ya
nchi yetu, ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za kuwekeza katika sekta
mbalimbali ili Tanzania ifikie azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati
ifikapo 2025.
Tags
KISWAHILI/ NJE