Jumla Watu 1,945 wamefariki dunia katika ajali za bodaboda 5,418 tangu
mwaka 2015 hadi Februari mwaka 2017 hivyo serikali imeanzisha mikakati
kabambe ya kupunguza ajali hizo ambazo zinapoteza nguvu kazi ya taifa
licha ya kutoa ajira nyingi kwa vijana
Akitoa mikakati ya Serikali jana Bungeni Mjini Dodoma Waziri wa Mambo ya
Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba, amesema kati ya mikakati hiyo ni kupitishwa
kwa kanuni ya leseni ya pikipiki na bajaji pamoja na kutoa elimu ya
usalama barabarani mashuleni pamoja na vyombo vya habari.
Mhe. Mwigulu amesema kuwa mikakati mingine ni kufanya ukaguzi wa mara
kwa mara kwa waendesha bodaboda, kuimarisha usimamizi wa sheria za
barabarani pamoja kusisitiza matumizi ya kofia ngumu ili kupunguza
madhara pindi ajali zinapotokea.
Aidha Waziri wa Mambo ya Ndani amesema kuwa Serikali kupitia wadau
mbalimbali nchini pia wanaendesha semina mbalimbali kwa waendesha
bodaboda hao ili kupunguza ajali lakini pia amelitaka suala hilo lianzie
kuelimishwa kuanzia ngazi ya jamii ili kulidhibiti kabisa.
Tags
ajali ya pikipiki