“Serikali inaficha jambo kuhusu Dreamliner 787-8, Tunaambiwa kwamba
Ndege tunayonunua Boeing 787-8 Dreamliner Ndio kwanza inaundwa. Sio
Kweli. Ndege hiyo iliundwa mwaka 2009 na kinachofanyika Sasa ni
kubadilisha Injini yake Kwa sababu Injini za ndege hizo zilikuwa na
matatizo ya kuwaka moto ( imetokea Kwa Ethiopian na Nippon Air ya Japan
). Hivi sasa kuna ushindani mkubwa kati ya Kampuni ya GE ya Marekani na
Kampuni ya Rolls Royce Uingereza kuhusu nani apate biashara ya injini
hiyo.
Hata hizi Bombardier tulizonunua hazikuundwa baada ya sisi kuweka order.
Ndege hizi ziliundwa mwaka 2014 na zilikuwa tayari zimenunuliwa na
Kampuni ya ndege ya Kazakhstan kabla ya baadaye kuuziwa sisi. Ushahidi
wa hili ni rahisi Sana, ukipanda ATCL Bombardier tafadhali soma
maandishi madogo dirishani utaona S/N 0001519017-040 DATE 10/2014. Hiyo
10/2014 ni Oktoba, 2014.
Serikali inaficha jambo katika suala la ununuzi wa Ndege hii ya
Dreamliner. Serikali inajua kuwa imenunua Terrible Teen Kwa bei kubwa
kuliko ilivyostahili. Shirika la ndege la Boeing linajua kuwa wametupiga
bei ya kuruka na kutudanganyia Kwa kubadili injini. Serikali inajua
kuwa haikusimamia maslahi ya Taifa katika mazungumzo kuhusu bei. Bahati
mbaya Sana mazungumzo hayo yalimhusisha Rais John Magufuli na Katibu
Mkuu Fedha James Doto peke yao. Hapakuwa na Government Negotiation Team
Kama ilivyo kawaida ya manunuzi makubwa ya namna haya.
Shirika la Boeing wametumia uzoefu wetu mdogo kutupiga na Ni wajibu wa
Watanzania wote Kwa kutumia mahusiano yetu yote duniani kuwataka Boeing
wawajibike kwa udanganyifu wao kwetu. Boeing wanapaswa kurudisha sehemu
ya Fedha yetu. Ni aibu Kwa Kampuni kubwa Kama Boeing kuiibia Nchi
masikini Kama Tanzania. Watanzania mnakumbuka sakata la Radar? Hii ni
kurushwa zaidi ya radar. Hela zetu zirudi tujenge Reli au kuongeza
Ndege.
Zitto Kabwe
3/5/2017
