
Na Benny Kisaka
Abdulkarim Omary Mtiro, almaarufu Cisco Mtiro, umelala Brother tangulia.
Umelala
usingizi. Usingizi ambao hautaamka wakati huu. Hautaamka brother kwa
kuwa wanaolala usingizi huu wanamngoja aliyewaumba awaamshe.
Kwa neema yake kuu iko siku utaamka Brother. Mara hii ukiamka hutalala tena.
Naam,
hutalala. Maana utakuwa umevuka ng’ambo ya pili ya mto. Huko hakuna
uchungu na maumivu makali kama uliyoyapitia nyakati zako za mwisho za
uhai wako ukiwa hospitali ya Aga Khan. Pumzika kaka yetu.
Leo
June 7, saa 7 mchana tunakuzika kwenye makaburi ya Kisutu mahali ambapo
miezi michache iliyopita tulimzika rafiki yako wa karibu Afande Chicco.
Pumzika kwa amani, mpaka tutakapoonana tena huko juu Ng’ambo ya pili.
Mwanadiplomasia uliyewahi kuwa balozi mdogo Nigeria na pia Balozi Kamili nchini Malaysia.
Tunakuita brother kwa wakazi wa Temeke tukijua umezaliwa peke yako kwa Mzee Omary na Bi Ummi Seif.
Akiwa
amezaliwa mtaa Kipata Kariakoo mwaka 1950, baada ya miaka miwili
alihamia Temeke hadi anamaliza elimu ya Chuo Kikuu, alihama pale
alipoanza kazi wizara ya mambo ya Nje.
Cisco
ni jina la utani lililochepua hadi kuliweka rasmi hata kwenye passport
yake ikisomeka Abdul Cisco Mtiro amefariki akiwa na miaka 67.
Leo Temeke itanyanyuka eneo ulilokulia na kusoma elimu yako ya msingi shule ya Temeke, na kumaliza elimu hiyo mwaka 1965.
Itakumbukwa
1997 aligombea Ubunge Temeke akishindana na Mrema, viongozi wote wa
ngazi za juu wa CCM walikuja kukupigia debe lakini kura hazikutosha.
Umaarufu wako upo Chang’ombe, Ilala, Wailes, Kurasini Masaki, Magomeni, Mbezi Beach, Kariakoo na hata Kinondoni yote.
Ameishi
Mikocheni B hadi umauti umemkuta, lakini muda mwingi amekuwa akikutana
na marafiki zake viunga vya Kinondoni kwa John Fedha ama nyuma ya
ubalozi wa Ufaransa kijiwe cha Octa.
Ni
mmoja wa waanzilishi wa bonanza la kila jpili pale Leaders Club,
mshabiki mkubwa wa Yanga, rafiki wa kila tabaka na rika na hakuwa mtu wa
kujikweza, umaarufu wake ulitawala kwa kuwa mtu mwenye utani mwingi…
Ni mtoto wa mjini hasa, hakuhitaji aimbwe redioni kutokana na sababu zozote.
Nilikuwepo
Kisutu kukuzika bro, ulishiriki msiba wa baba yangu Christopher kisaka,
ambaye alikuwa mwalimu wako shuleni Temeke, ulitukaribisha nyumbani
kwako kupata chakula cha jioni mara kadhaa tulipofika Kuala Lumpur,
Malaysia 2011 nikiwa na Juma Pinto, ulinialika arusi ya mwanao Omary,
pia nilishiriki.
Mwanadiplomasia, mkuu wa Itifaki mstaafu kwa Mwalimu Nyerere, Mzee Mkapa na awamu ya nne ya Jakaya Kikwete.
Ulikuwa mgeni rasmi miss Temeke 2003. Ulikuwa judge miss Tanzania 2004.
Cisco
ana marafiki lukuki kiasi kila mmoja anaweza kumwandika amjuavyo, tena
zaidi na vizuri kutipa mimi, ila kwa udogo huu naomba mwenyezi Mungu
akupumzishe kwa Amani
Tags
TANZIA
