Hatimaye Rais Donald Trump ametangaza kuiondoa Marekani kutoka
makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyoafikiwa na kutiwa
saini mwaka 2015 mjini Paris, Ufaransa ikiwa ni mojawapo ya ahadi
alizotoa wakati wa kampeni.
Katika hotuba yake kali aliyotoa kutoka Ikulu ya White House, Trump
alisema Marekani itasitisha mara moja utekelezaji wa makubaliano ya
Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Huku akitumia kauli mbiu ya ‘Marekani Kwanza’ ujumbe aliotumia wakati wa
kampeni zilizomwingiza Ikulu mwaka jana, Trump alisema Mkataba wa Paris
utahujumu uchumi wa Marekani, utawafanya wananchi kupoteza kazi,
kudhoofisha uhuru na kuiweka nchi hiyo milele katika hali ya kutumiwa na
mataifa mengine duniani.
Trump alisema Wamarekani hawataki viongozi wengine na nchi nyingine
kuwacheka, na hataruhusu hilo. Alisema mkataba huo uliosainiwa wakati wa
utawala wa mtangulizi wake Barack Obama, unawaweka katika nafasi nzuri
wapinzani wa nchi hiyo kiuchumi ambao ni India, China na Bara la Ulaya
Wapinzani wake wanasema hatua ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba huo
ni sawa na kuyakimbia majukumu yake kama kiongozi katika kukabili
changamoto hiyo inayoikabili dunia.
Trump hakutoa maelezo kuhusu ni vipi au lini mchakato rasmi wa kujiondoa
utaanza, na kwa wakati mmoja aliashiria kuwa mazungumzo mapya huenda
yakafanyika. Hata hivyo wazo hilo lilipingwa na viongozi wa Ulaya
waliojawa hasira, ambao waliungana na viongozi kutoka kote Marekani
kulaani hatua ya Trump.
Katika taarifa ya pamoja, Ufaransa, Ujerumani na Italia zimesema makubaliano hayo hayawezi kujadiliwa upya.
Tags
Donald Trump
