
Pengine ni katika harakati za kuutafuta utanashati au ukosefu wa
ajira, na huenda ikawa ni mtindo wa kimaisha kwa vijana wengi hapa
nchini na duniani kote wanaotunisha misuli. Hata hivyo wanaume walio
katika harakati za kutunisha misuli au kupata maumbo yenye miraba minne,
wamekuwa wakitumia dawa ili kuyapata maumbo hayo badala ya kufanya
mazoezi ya viungo.
Vijana wengi hivi sasa wananunua kwa wingi dawa za kutunisha misuli
maarufu kama ‘doping’ kwa sababu zinazotajwa kuwa ni kutafuta ajira kama
vile ulinzi kwenye kumbi za starehe, ulinzi wa watu maarufu(bodyguard)
na wengine mashindano ya kunyanyua vitu vizito huku wengine wakiutafuta
utanashati.
Steroids
Wataalamu wa afya wanataja baadhi ya dawa zinazonunuliwa na wajenga
misuli kuwa ni Anabolic Steroids, ambazo husaidia kujaza misuli na
kutochoka haraka.
Ripoti ya Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani inaeleza hivi:
“Dawa za steroids za kuongeza ukubwa wa misuli ni kemikali zinazohusiana
na homoni za kiume (tetosterones). Dawa hizo huchochea ukuzi wa misuli
na kustawi kwa maumbile ya kiume. Wavulana wanapobalehe homoni hizo
huongezeka na kubadilika na hivyo kuchochea mabadiliko ambayo humfanya
mvulana awe mwanamume. Nyingine ni Creatine ambazo huuzwa katika hali ya
unga unga na kama ilivyo Steroids, dawa hii nayo hujenga misuli na
kuondoa maumivu ya mwili na Human Growth Hormone, vichocheo ambavyo
hukuza misuli ya mtu kwa wiki chache tu.
Dawa nyingine zenye nguvu na zinazotumiwa zaidi na wanaume wanaotaka
kujenga misuli ni Optimal Stack, Precision Power, Estoforce Edge, Muscle
Ex Edge na Muscle Rip Edge.
Miaka ya 70, watunisha misuli wengi akiwemo Arnold Schwazenerger,
walikiri kutumia Steroids kama dawa zinazowasaidia kukuza misuli yao
hata hivyo mwaka 1990, Marekani, ilianzisha sheria ya kuzuia dawa za
Steroids na kuiweka katika kundi la dawa zilizopigwa marufuku.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya vijana hutumia dawa za
vichocheo vya wanaume kama testosterone kukuza misuli hiyo. Wengi
hutumia dawa hizo kwa kiwango kikubwa kiasi cha mara 10 hadi 100 zaidi
ya kile ambacho daktari anaweza kukuandikia.
Wengi huzipata dawa hizi nchini Afrika Kusini ambako huletwa na watu
binafsi na kuzisambaza katika nyumba za mazoezi (gym) ambako vijana
wengi hufanya mazoezi ya kujenga vifua.
Gosbert Msuya, mlinda mlango wa klabu ya muziki ya Maisha, anakataa
kutumia dawa za kutunisha misuli, lakini anakubali kuwa wapo vijana
wanaotumia dawa hizo kwa sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni ajira na
mwonekano. “Sasa ukiwa na mwili mkubwa unapata kazi za kuwalinda watu
maarufu, kulinda ‘stage’ pindi wanamuziki wanapoburudisha. Ajira
nyingine ni wakati wa maadhimisho makubwa ya kitaifa, kucheza filamu, na
mwonekano mzuri,” anasema Msuya.
Kijana anayekunywa dawa hizi huweza kuongezeka kilo tano hadi 15 ndani
ya miezi miwili. Mzunguko na msukumo wa damu yake huongezeka kiasi cha
asilimia 20, jambo linalosababisha misuli yake kujaa.
Misuli hii huonekana wazi zaidi kwani dawa hizi husaidia kuchoma kalori
kwa kiasi kikubwa n husababisha mwili kupoteza mafuta mengi.
Madhara
Madhara yanayoweza kuwakuta vijana wanaotunisha misuli kwa kutumia
vidonge vya vichocheo au steroids ni pamoja na maradhi ya moyo, lehemu
mbaya mwilini, chunusi, upara, mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo, ini
na figo huweza kuharibika. Wengine huweza kupata matiti kama ya
mwanamke. Kwa upande mwingine, wanawake wanaotumia dawa hizi hupata
sauti za kiume na ndevu. Mengine ni kukosa uwezo wa tendo la ndoa,
kusinyaa au kupotea kwa korodani, tezi dume kukua, kuwa na hasira,
shinikizo la damu.
Madhara mengine ni ogani muhimu kushindwa kufanya kazi ghafla, kama vile
ini. Kifo cha ghafla, saratani na figo kushindwa kufanya kazi. Lakini
pia, wataalamu wanasema wengi wanaotumia dawa hizi hugeuka kuwa wajeuri
na wenye hasira za haraka.
Namna ya kumfahamu anayetunisha misuli kwa dawa
Ingawa ni vigumu kumfahamu mtu anayetumia dawa za kutunisha misuli kwa
asilimia 100 hasa kwa wale ambao hawajatumia dawa kwa muda mrefu, lakini
unaweza kumfahamu mtu aliyetumia dawa hizo.
Kwanza wengi hupata misuli mingi kwa wiki chache, na misuli yao hujitokeza nje ya ngozi kama imepigwa ‘pampu’.
Hata hivyo wataalamu wa afya wanasema, misuli ya mtu anayetumia dawa si imara kama ya mtu anayefanya mazoezi.
Watunisha misuli waliopatwa na vifo vya ghafla
Inasadikiwa kuwa asilimia kubwa ya watunisha misuli hawa, walifariki
dunia ghafla kutokana na dawa za kutunisha misuli na wakati mwingine
wakizichanganya na dawa za kulevya. Wa kwanza ni Carlos Rodrigues,
Mohammed Benaziza, Chuck Sipes, Ray McNeil, Andreas Munzerm, Sonny
Schimidt, Don Youngblood na Paul Demayo.
Mfamasia katika Hospitali ya Mirrs ya Mwenge, David Cyprian anasema,
kikubwa kinachofanywa na watunisha misuli ni matumizi mabaya(abuse),
ambapo dawa zinazotumika kufanya kitu kingine hutumiwa kujenga misuli.
Anatoa mfano kuwa, dawa za vichocheo vya kiume(testosterone) na
Steroids, zina kazi ya kuwasaidia watu wanaochelewa kupata balehe, wenye
matatizo ya ugumba na waliopoteza uzito mkubwa kwa sababu ya maradhi ya
HIV.
“Hata wanariadha nao hutumia dawa za aina hii kwa sababu ya kuongeza
nguvu na kujenga misuli. Lakini ili kupata uhakika iwapo mtu ametumia
dawa za aina hiyo, mkojo wake hupimwa” anasema.
Mlinzi Mkuu wa Ukumbi wa Swispub, Tabata na mwalimu wa mazoezi, Selemani
Bwagege anashauri vijana kufanya mazoezi na kufuata nidhamu ya mazoezi
badala ya kutumia dawa.
“Mambo mengine tunayaiga ingawa hayana umuhimu kwetu kiafya. Ukifanya mazoezi unapata umbile kubwa na langu,” anasema.
Anakiri kuwa, vijana wengi wanaotaka miili mikubwa wanafanya hivyo kwa ajili ya ajira.
Zifahamu dawa za Steroidi
Mfamasia wa Msuya anaeleza kuwa Steroidi zilitengenezwa viwandani kwa
mara ya kwanza katika miaka ya 30 ili kuwatibu wanaume ambao walishindwa
kutokeza homoni za kutosha. Leo, steroidi hutumiwa kurekebisha
kudhoofika kwa mwili kunakosababishwa na virusi vya Ukimwi na magonjwa
mengine.
“Hata hivyo, Steroidi hutumiwa sana na watu wasio na uhitaji wa kitiba.
Katika miaka ya 50, steroidi zilianza kupatikana kimagendo, na
wana-michezo waliojitakia sifa walianza kuzitumia kuongeza nguvu
mwilini,” anasema.
TFDA wazungumzia dawa hizo
Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza anasema
dawa za kutunisha misuli zinaingia nchini kwa utaratibu wa uingizaji wa
dawa na kabla ya kusajiliwa hupitia maabara na kupimwa.
Hata hivyo, anasema dawa hizo zinapotumika bila kuandikiwa na daktari na
kutumiwa kiholela, huweza kusababisha madhara ingawa zikitumika kwa
sababu husika madhara ni madogo, lakini zikitumiwa kwa sababu nyingine
husababisha madhara.