
Ndoa inatajwa kuwa ni elimu pekee ambayo mtu anapata cheti kabla ya kuingia darasani.
Licha ya misukosuko mingi iliyomo ndani yake ndoa imeendelea kuwa tukio
muhimu katika jamii zote duniani na kurithishwa kwa vizazi na vizazi.
Moja ya misukosuko ya ndoa ni uaminifu, ambao baadhi yao wametokea kuukosa na kusababisha nyingine kuyumba au kufa kabisa.
Wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani walijadili suala hili la hilo na kuja na dalili tano za wanandoa wasio waaminifu.
Kuchukia majukumu ya msingi ya ndoa
Watalaamu wanaeleza kuwa dalili mojawapo ni mwanandoa kutopenda kufanya mambo na kazi za familia.
Mtaalamu wa masuala ya ndoa kutoka Marekani Jeannie Ingram anayefanya
shughuli za kutoa ushauri wa kindoa eneo la Nashville, Tennessee anasema
zipo sababu nyingi za mmoja wa wanadoa kutoka nje ya ndoa, ikiwamo
kutoshirikiana kwenye masuala mengi yakiwamo ya kifamilia.
Anasema mara nyingi mwanandoa anayetoka nje ya ndoa hana muda wa
kusikiliza familia ina tatizo au furaha gani. Anafafanua kuwa hiyo
inatokana na muda wote kufikiria mambo ya familia nyingine hata kama ni
ya mtu huko alikoanzisha uhusiano.
“Akiwa anatoka nje ya ndoa hana muda wa kupoteza kufikiri vitu vingine
zaidi ya mambo yake na jinsi atakavyokutana na mtu au watu wake
anaoshirikiana nao kwenye usaliti, ” anasema Ingram.
Kuchukia kushiriki tendo la ndoa
Anasema wengi wao hufanya mapenzi na wenza wao kwa kujilazimisha na wakati mwingine kulazimishwa kwa uwazi kabisa.
“Wakiwa siyo waaminifu , hawavunjia pia uhusiano na wenza wao,
aliliambia Jarida la HuffPost, ukweli ni kwamba uhusiano wa kindoa
unahitaji kuimarishwamara kwa mara.
“Kukutana kimwili ni mojawapo ya mambo yanayopandisha mapenzi na kuamsha
hisia ya kila mmoja wao kutamani kushiriki tendo hilo, jambo ambalo
huwafanya kuwa pamoja muda wote ”anasema Ingram.
Wanatumia muda mwingi pamoja, lakini kila mmoja anafanya lake
Mtaalamu wa saikolojia kutoka Marekani Jimbo la Cororado Aaron Anderson
anaitaja sababu ya kwanza kuwa ni pamoja na kutumia muda mwingi wakiwa
pamoja, lakini kila mmoja ana shughuli zake ikiwamo kuchezea simu,
kufungua kompyuta mpakato na kufanya kazi.
“Kama wewe na mke wako mnatumia muda mwingi katika chumba kimoja lakini
kila mmoja ana shughuli zake na hakuna jambo lolote mnalojadili kuhusu
uhusiano wenu mmoja au wote wawili mnatoka nje ya ndoa,” anasema
Anderson.
Anasema siyo jambo la kawaida kwa wanandoa wanaopendana kutumia saa mbili kila mmoja akiperuzi kwenye mitandao ya kijamii.
Anasema kwa kawaida wapendanao wanapokaa wawili kila mmoja huzima simu, kompyuta na kuzungumza na mwenzake kwa namna yoyote ile.
“Hili halihitaji darubini huja lenyewe bila kufahamu, kuna ambao wakiwaona wenza wao husahau kila kitu , ”anasema.
Hawashirikiani katika mipango ya “mitoko” ya mwisho wa juma
Licha ya kuishi nyumba moja lakini kila mmoja hupanga mipango yake ya namna atakavyomaliza mapumziko ya wiki.
Mmoja wa wanandoa Said Miraji anasema kuwa alipomuoa mkewe ilikuwa
kawaida mkewe kumlazimisha amsindikize hadi anapokwenda kutengeneza
nywele.
Anasema baada ya kupata mtoto mmoja mambo hayo yalipungua na hatimaye kwisha kabisa.
“Nilipochunguza baada ya mambo ya kutaka kujitenga kuzidi, nilichobaini
sitaki kusema, ninachoweza kukuambia ni kuwa ameolewa na mwanamume
mwingine na ana watoto wawili na mimi kaniachia wawili ”anasema Miraji.
Kauli ya Miraji inaungwa mkono na mwanandoa mwingine Kuruthumu Rajabu
anayesema kuwa mabadiliko yakitokea ndani ya ndoa mwisho wake ni
kuachana.
Anasema baada ya kukaa kwenye ndoa na mumewe kwa miaka minne mwenza wake huyo alianza tabia ya kuchelewa kurudi isivyo kawaida.
Anasema mbali ya hilo, pia alikuwa hali chakula cha nyumbani, hajulikani
anapumzika lini, kwa sababu kila siku anakwenda kazini, kibaya zaidi
alikuwa hataki hata kuongozana naye.
“Ilifikia mahali hata nikimsubiri hatuwezi kwenda kulala pamoja lazima
atatafuta kisingizio abaki sebuleni na kuja kulala kwa muda wake”anasema
Kuruthumu.
Anasema licha ya kuwa mama bora, mcha Mungu, anayejali familia ya pande
zote na kujaribu kuvumilia mapungufu ya mumewe, “Tuliishia kuachana,
haikuwa kazi rahisi kumbadili alichoka manung’uniko yangu akaniacha”.
Hawaulizani hali, safari zinaongezeka
Anderson katika andiko lake alilochapisha kwenye jarida la Le wedding
magazine la Ufaransa anasema kuwa ni nadra kwa mwanandoa anayetoka nje
ya ndoa kumuuliza mwenzake habari za atokako hata kama amesafiri mwezi
mzima.
“Anaweza asiulize hali za watoto pia bila kujali ni mwanamume au
mwanamke, kwa sababu anawaza vitu vingine na kuchukia kwa nini aliolewa,
” anasema.
Anasema mwenza anayetoka nje ya ndoa muda mwingi anakuwa mtu wa safari za ndani au za nje ya eneo analoishi.
Huwasimanga au kuwasema vibaya marafiki, ndugu wa mwenza wake.
Kungwi maarufu Chausiku Salumu Maele maarufu Bi Chau anasema kuwa mbali
na mabadiliko ya aina zote, kikubwa mwanandoa anayetoka nje ya ndoa
huwachukia marafiki na ndugu wa mwenza wake.
Anasema anaweza kuwasema vibaya wakiwepo au pembeni.
“Huona kama wanaingilia uhuru wake wa kumbeza mume au mke, hivyo huwachukia na hutamani wasiwepo maisha.
“Ikitokea kwa bahati mbaya akapishana maneno ya mmoja wa watu hao kamwe
hatomsamehe na huliweka hilo kama kosa kubwa maishani, ”anasema Bi Chau.
Anasema kuwa mwanandoa asiyemwaminifu pia huwa mgumu kujadili migongano
ya ndani ya ndoa na akiulizwa hujibu “Sina muda wa kujadili suala hilo”.
Anasema kumsoma mwenza wako na kutambua mabadiliko ya tabia yake ni jambo muhimu ili kukwepa kuvunjika kwa ndoa.
Anafafanua hajawahi mwanaume au mwanamke kutoka nje ya ndoa na mpenzi
mmoja kwa miaka miwili mfululizo na ndoa yake ikawa salama.
“Njia pekee ya kunusuru ndoa ni wanandoa kujuana tabia, kujibizana
maswali panapotokea sintofahamu. Kukaa kimya na kupuuzia hisia kumekuwa
chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa nyingi, ”anasema Bi Chau.
Anachosema Bi Chau kinashadidiwa na Anderson anayesema mwanandoa
anayetoka nje ya ndoa pia hana mapenzi na familia ya mmoja wao. Pia ndoa
iliyoingia usaliti wanandoa huwasema vibaya marafiki wa wenza wao,
kuwakashifu na kuwadhihaki.
“Ujue hapo hakuna ukweli kuna usaliti unaendelea kuwa makini, ”anasema Whetstone.
Mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (MUHAS) Lusajo Kayula anasema kila ndoa au uhusiano una tabia
yake ambayo wahusika wameizoea.
Anasema kwa sababu hiyo mabadiliko ya mwanandoa asiye mwaminifu hutegemea na mazoea yao.
Anafafanua kuwa dalili, tabia za mmoja kati yao anayetoka nje ya ndoa
hulingana na walivyozoea ndiyo maana siyo rahisi kufanana kutoka ndoa
moja na nyingine.
“Zipo tabia tofauti ambazo zinatia shaka ikiwamo kuwa makini na simu
zaidi ya kawaida, kutotaka ukaribu na mwenza wake na kupoteza hamu ya
tendo la ndoa kwa mwanandoa mwenza, ”anasema Kayula.
Kayula anafafanua kuwa zipo dalili nyingine ambazo mwanandoa anaweza kuwa nazo na bado asiwe anatoka nje ya ndoa.
Anafafanua kuwa wengi wanaamini mwanandoa anayechelewa kurudi nyumbani
anakuwa na uhusiano, “Wapo wanaorudi saa 11 jioni na bado wanatoka nje
ya ndoa, hicho siyo kigezo.
Anaeleza hata kupoteza hamu ya tendo la ndoa siyo kigezo kwa sababu wapo wanaopoteza kwa sababu ya msongo wa mawazo.
“Ndiyo maana nilisema hapo mwanzo hutegemea wahusika walizoea nini, kimetokea nini kwenye maisha yao, ”anasema.
Baadhi ya sababu za kutoka nje ya ndoa
Bi Chau anazitaja baadhi ya sababu za kutoka nje ya ndoa kuwa ni pamoja
na wanandoa hususani wanawake kuaminishwa kuwa moja ya jukumu lao ni
kuficha siri za ndani ya ndoa.
Anasema iwapo watatoka na kutafuta tiba ya matatizo mbalimbali
yanayowakuta ndani ya ndoa hali hii haitakuwepo, “Sitaki kukudanganya
tatizo la kutokuwa na nguvu za kiume limekuwa kubwa.
“Wanawake hawawezi kulalama kuhusu hilo matokeo yake wanakuwa watumwa wa
ngono, wanaume nao halikadhalika, kutokana na kutoka nje ya ndoa
wanapunguza mapenzi kwa wake zao na hatimaye kutotamani kukutana nao na
kuwa watumwa wa mapenzi wa nje ya ndoa, ”anasema.
Anafafanua kuwa hizo ni baadhi ya sababu, zipo nyingi na zinahitaji kutafutiwa majibu na wanandoa wote.
“Kiukweli hili ni jinamizi, hakuna ambaye yupo salama, wanandoa wengi wanatoka nje ya ndoa zao, ili usiwe mmoja wao kuwa makini.
“Dawa ni kusema, kujadili kukubaliana , kueleweshana kwa pamoja badala ya kila mmoja kumuona mwenzake mkosaji, ”anasema.