
SIKU chache baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Uganda, Ivan
Ssemwanga ‘Ivan Don’ kuzikwa, aliyekuwa mkewe Zarina Hassan ‘Zari the
Boss Lady’ ameeleza namna alivyokiona kifo cha Ivan Don.
Akizungumza na mtandao mmoja wa burudani, Zari alisema alipewa taarifa na madaktari mapema baada ya hali ya Ivan kubadilika.
Zari alikuwa akijibu swali aliloulizwa na mtandao huo iwapo tetesi kuwa aliyekuwa mumewe Ivan alikufa kwa sumu au lah.
“Ivan alikuwa na presha ya kupanda na hakuwahi kupima… na kama alipima hakuwahi kuichukulia serious na kuanza kutumia dawa.
“Kilichotokea ni kwamba alipata kiharusi, hapo presha nayo ikapanda…
presha ikiwa juu, akapooza upande mmoja wa mwili wake ambao ulikuwa wa
kushoto.
“Kiharusi kilimpiga vibaya, akapasuka mshipa kichwani ambao ulimwanga
damu kwenye ubongo. Madaktari wakaniambia asilimia kubwa ya wagonjwa wa
aina yake, asilimia 80 hufariki dunia mara moja.
“Asilimia 20 inayobaki, asilimia kumi huweza kufariki ndani ya mwezi
mmoja na asilimia kumi nyingine; kama wakibahatika kupona huwa hawawezi
kufanya chochote tena. Ni wa kuwavalisha pempasi, kuogeshwa, kulishwa na
nk,” anasema Zari.
Zari anaongeza: “Baadaye wakaamua kumfanyia upasuaji lakini
haikufanikiwa kwa sababu presha yake ilikuwa inapanda na kushuka kila
wakati, wakamrudisha wodini kujaribu kumsaidia kwa njia nyingine.
Anasema siku mbili baadaye alipigiwa simu na daktari akamwambia aende kumuaga Ivan kwa sababu hali yake haikuwa nzuri.
Presha yake ilikuwa ikipanda hadi kufikia 220, badala ya kiwango cha
kawaida cha 120 – 125, hali ambayo Zari anaielezea kuwa madaktari
walimwambia haikuwa nzuri.
“Siku anafariki, nilipigiwa simu mida ya saa mbili usiku, nikaambiwa
kwamba Ivan amefariki. Lakini siku moja kabla tulielezwa hilo na
tulizuiwa kumtembelea wodini maana alikuwa kwenye process ya kufariki.
Tukashauriwa tumwache apumzike akiwa kwenye hali ya utulivu.
“Tuliambiwa tumuage, tukafanya hivyo. Siku hiyo iliisha bila taarifa
yoyote hadi siku iliyofuata saa mbili usiku. Kwahiyo siyo sumu, Ivan
amekufa baada ya mshipa wa kichwani kupasuka na kusambaza damu kwenye
ubongo, pamoja na kiharusi,” anasema Zari.
MAMBO YALIYOZUA GUMZO MSIBANI
Ivan Don alizikwa Jumanne wiki hii, katika makaburi ya ukoo, kijijini
kwao Kayunga, nje ya jiji la Kampala, Uganda ambapo walihudhuria maelfu
ya watu wakiwemo mastaa wa Uganda na nchi jirani.
Kwa hakika maziko ya Ivan Don ambaye alikuwa kiongozi wa Kundi la Uganda
Rich Gang Family, yamedhihirisha namna alivyokuwa na utajiri wa mali
na watu wenye mapenzi mema naye.
Yametokea mengi kwenye msiba huo, lakini hapa utaona yale yaliyozua gumzo zaidi siku na wakati wa msiba wake.
DIAMOND KUTOHUDHURIA
Mpenzi wake na Zari, mwanamuziki Diamond Platnumz aliahidi kuhudhuria maziko hayo, lakini hakuweza kufanya hivyo.
Jambo hilo lilizua gumzo kubwa mitandaoni kwani wengi waliamini angefika
kutokana na ahadi yake lakini hata namna alivyoonyesha utu na kujali
kiasi cha kumruhusu Zari kusafiri hadi Sauzi alipokuwa akipatiwa
matibabu kabla ya kifo chake.
Hata hivyo Meneja wa Diamond, Sallam SK alisema walipanga Diamond ahudhurie maziko hayo, lakini ratiba ziliingiliana.
Anasema walipanga Diamond aingie huko Alfajiri ya Jumanne, lakini ndugu
wa marehemu wakaamua kusafirisha mwili usiku wa Jumatatu hivyo mipango
ikavurugika.
AZIKWA NA FEDHA
Katika kile kilichoonekana kufuru, wakati mwili wa Ivan ukiwa tayari
kaburini, marafiki wa marehemu Ivan, matajiri wa Uganda walianza kutupia
fedha kaburini.
Ni kama vile walikuwa wakimtuza mtu, lakini ukweli ni kwamba walikuwa
wakimwaga fedha kaburini, jambo ambalo lilizua maswali mengi kuliko
majibu.
BIASHARA MSIBANI
Kwenye eneo la msiba kulikuwa tofauti kabisa na misiba mingine; msiba wa Ivan ulikuwa maalum na wa kistaa.
Wafanyabiashara wadogo walitumia nafasi hiyo kutengeneza fedha kwa kuuza
vyakula, tisheti, kofia na vipeperushi vyenye picha na maelezo kidogo
juu ya marehemu.
ZARI ATUKANWA
Wakati shughuli za msiba huo zikiendelea, Zari alikuwa akiposti picha na
maelezo kwenye ukurasa wake wa Instagram ili kuwaonyesha wadau
kinachoendelea, lakini wapo ambao hawakumuunga mkono na kumtolea lugha
sizizo na staha.
Hata hivyo, mwigizaji wa Bongo, Wastara Juma alijitosa kumtetea ambapo alisema wanaomsema vibaya Zari wamekosa utu.
“… mimi ni mama sijawahi kusahau uchungu wa mwana na wala sijamsahau
aliyenifanya niitwe mama lakini usiniulize kwanini sipo na niliyezaa
naye ni mambo binafsi sana sio lazima kila mtu ajue lakini akifa
nitaenda na ikibidi kulia nitalia sababu alikuwa na bado atakuwa baba wa
watoto wangu…
“Lakini why why why mtu atukanweee weee asemwee kipindi kibaya cha
uchungu na mawazo kama hiki? Hivi jamani mnajua kufiwa kweli wenzangu,
mbona hili la Zari kutukanwa limenishinda kabisa kuvumulia. Mungu amlaze
mahali pema Ivan – Amen.”
MTOTO MWINGINE WA IVAN
Baada ya kifo cha Ivan, imeelezwa kuwa mbali na watoto watatu aliozaa na
Zari (Pinto, Didy na Quincy), ana mtoto mwingine mmoja wa kike.
Akifafanua hilo, Zari alisema ni kweli Ivan anaye mtoto huyo lakini siyo
wa kumzaa bali alimuasili kutoka kwa kaka yake ambaye alifariki kwa
kupigwa risasi na majambazi waliokuwa wakijaribu kumwibia Zari, ndipo
Ivan kwa heshima akaamua kumuasili mtoto huyo kwa vile baba yake
alifariki akipigania familia yake.
Tags
Zari Hassan