Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Serikali imebuni vyanzo vingine
vya mapato ili kupanua wigo wa kodi kwa ajili ya maendeleo endelevu
nchini na kukuza uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha bajeti ya Serikali
kwa Mwaka wa Fedha 2017/18 Bungeni mjini Dodoma, waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa Serikali itaendelea na
ukusanyaji wa kodi ya majengo (yaliyothaminiwa na yasiyothaminiwa)
kwenye halmashauri zote nchini.
Ameongeza kuwa jukumu hilo
litasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Mamlaka ya Mapato
Tanzania. Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango
vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo
hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate) cha
shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na shilingi elfu hamsini (50,000)
kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
“Serikali itawatambua rasmi
wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika
maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza
mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika
kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya”, alisema Dkt.
Mpango.
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa
Serikali itaendelea kusimamia na kuhimiza matumizi ya mashine za
kielektroniki (EFDs) kwenye Wizara, Idara, Taasisi za Serikali na kwa
wafanyabiashara.
Ili kudhibiti mapato yatokanayo na
madini, Dkt. Mpango amesema Serikali haitoruhusu usafirishaji wa madini
kutoka migodini na kupeleka moja kwa moja nje ya nchi. Aidha, Serikali
itaanzisha maeneo maalum (clearing houses) katika viwanja vya kimataifa,
migodini, na kadhalika ambapo madini hayo yatathibitishwa na kupewa
kibali cha kusafirisha madini hayo ambacho kitatozwa ada ya asilimia
moja (clearing fee) ya thamani ya madini hayo.
Waziri huyo wa Fedha na Mipango
amesema Serikali itafungua akaunti maalum (Escrow Account) kuanzia mwezi
Julai 2017 ili kurahisisha na kuhakikisha kwamba marejesho ya Ushuru wa
Forodha wa ziada (Additional Import Duty) wa asilimia 15 unaolipwa na
waagizaji wa sukari ya viwandani yanafanyika kwa wakati. Hatua hii
itaiwezesha Mamlaka ya Mapato kufanya marejesho kwa wakati kwa
wazalishaji wanaotumia sukari hiyo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.
Dkt. Mpango amesititiza kuwa
Serikali itaimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa na
mifumo ya kielektroniki ili kuzuia uvujaji wa mapato ya Serikali.
“Mfumo uitwao “Government
e-payment Gateway System” uko tayari kwa ajili ya matumizi ya Wizara,
Idara na Taasisi za Serikali. Wizara, Idara na Taasisi zote za Serikali
zinaagizwa zianze kutumia mfumo huu”, alisema Dkt. Mpango.
Amebainisha pia kuwa Serikali
imezindua mfumo mpya wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki
(Electronic Revenue Collection System (e-RCS)) ambao utadhibiti
udanganyifu unaofanywa na maafisa wa Serikali kwa kushirikiana na walipa
kodi katika kukadiria kodi sahihi. Aidha, mfumo huu utawasaidia walipa
kodi kwa kuwa na uhakika wa kiasi cha kodi wanayopaswa kulipa. Mfumo huo
wa e-RCS utaanza rasmi katika mwaka huu wa fedha kwa usimamizi wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
kwa upande wa Bara na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa upande wa
Zanzibar.
Katika mwaka 2017/18, Serikali
inapanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 31,712.0. Kati ya fedha hizo,
shilingi bilioni 19,712.4 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida,
ikijumuisha shilingi bilioni 7,205.8 za mishahara na shilingi bilioni
9,461.4 kwa ajili ya kulipia deni la umma na huduma nyinginezo. Aidha,
matumizi ya maendeleo yatakuwa shilingi bilioni 11,999.6 sawa na
asilimia 38 ya bajeti.
Tags
Pato la Taifa