Na: Mwandishi Wetu- MAELEZO
Kasi ya ukuaji wa uchumi nchini
imeendelea kuimarika ambapo Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi
tano barani Afrika zilizoongoza kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa
uchumi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti kwa
mwaka 2017/2018 bungeni leo, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip
Mpango amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu wa Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF), Tanzania inashika nafasi ya pili kwa ukuaji wa uchumi
ambapo uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.1 nyuma ya Ivory Coast ambayo
yenyewe uchumi wake unakuwa kwa asilimia 7.9.
Nchi zingine zilizokuwa na kasi
nzuri ya ukuaji wa uchumi ni Senegal (asilimia 6.6), Djibouti (asilimia
6.5) na Ethiopia (asilimia 6.5).
“Jarida la Benki ya Dunia
(Tanzania Economic Update) lililochapishwa Aprili 2017 linabainisha
waziwazi kuwa uchumi wa Taifa ni imara kwa kuangalia viashiria
mbalimbali kama ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, urari wa biashara,
akiba katika fedha za kigeni na thamani ya shilingi”. Alieleza Waziri
Mpango kwa kunukuu takwimu za Benki ya Dunia juu ya ukuaji wa uchumi
nchini.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio
yaliyoelezwa lakini bado kumekuwa na mijadala kuhusu afya ya uchumi wa
Taifa hususan ukwasi katika uchumi, kufungwa kwa biashara, na madai
kwamba sekta binafsi imepoteza matumaini na kujiamini (private sector
confidence) na kwamba hali hiyo imesababishwa na mambo mbalimbali
ikiwemo kuongezeka kwa mikopo chefuchefu katika mabenki.
“Takwimu pia zinaonesha kuwa
ukwasi wa mabenki ulianza kutetereka kutokana na kuongezeka kwa mikopo
chefuchefu kutoka asilimia 8.3 mwezi Machi 2016 hadi asilimia 10.9 Machi
2017 ikilinganishwa na kiwango kinachohitajika cha asilimia 5.
Alifafanua kuwa Mikopo kwa
sekta binafsi iliongezeka kidogo kwa asilimia 3.7 katika kipindi cha
mwaka ulioishia Machi 2017 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 23.6
katika kipindi kama hicho mwaka 2016.
“Kupungua kwa kiwango cha
ukuaji huo kulitokana kwa kiasi kikubwa na kuyumba kwa biashara duniani
ambako kuliathiri nchi nyingi duniani ikiwemo Tanzania”. Alifafanua Dkt.
Mpango.
Aidha katika bajeti hiyo, aliyataka mabenki yote nchini kusimamia kwa makini taratibu za kibenki katika utoaji wa mikopo.
Alieleza kuwa ili kuimarisha
ukwasi, Serikali kupitia Benki Kuu imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni
pamoja na kupunguza riba ambazo benki za biashara hukopa kutoka Benki
Kuu (Discount Rate) ili kuongeza ukwasi katika benki za biashara na
hivyo kuziwezesha kukopa kwa gharama nafuu zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri Mpango,
riba hiyo imepunguzwa kutoka asilimia 16.0 iliyokuwa ikitumika tangu
mwezi Novemba 2013 hadi asilimia 12.0 ambayo imeanza kutumika rasmi
tarehe 6 Machi 2017.
Aidha, ameeleza kuwa katika
kuimarisha zaidi soko la fedha nchini, Benki Kuu ilipunguza kiwango cha
amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki kuu kama
dhamana (Statutory Minimum Reserve Requirement – SMR) kutoka asilimia
10.0 hadi asilimia 8.0 ili kuziwezesha benki za biashara kuwa na ukwasi
zaidi kwa ajili ya kukopesha sekta binafsi na kwamba hatua hiyo imeanza
kutumika rasmi mwezi Aprili 2017..
“Ni matumaini ya Serikali kuwa
hatua hizi zitaziwezesha benki za biashara nchini kuongeza ukwasi wa
kutosha kuwakopesha wananchi kwa riba nafuu”. Alieleza.
Katika eneo la mazingira ya
kufanya biashara, Waziri mpango alieleza kuwa Serikali imeanza kuona
viashiria bora zaidi katika eneo la kuboresha mazingira ya biashara.
Amesema kwa mujibu wa taarifa ya
Benki ya Dunia ya mwaka 2017 ilionesha kuwa, Tanzania ilikuwa nchi ya
132 kwa urahisi wa kufanya biashara ikiwa imepiga hatua kwa nafasi 12
kutoka nafasi ya 144 mwaka 2016.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya
“Fahirisi ya Uwekezaji Afrika ya mwaka 2016” (Africa Investment Index,
2016) iliyotolewa na taasisi ya “Quantum Global Research Lab”
ya Uingereza, Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza miongoni mwa nchi za
Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji na ya nane kwa Afrika, ikiwa
imepiga hatua kutoka nafasi ya 19 mwaka 2015.
Tags
Uchumi