Na Jonas Kamaleki
Kati ya mambo ambayo yamekuwa
yakimuumiza kichwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ni ukusanyaji wa
kodi hivyo juhudi za makusudi zimefanyika ili kutimiza azma hii.
Serikali ya Awamu ya Tano
imetekeleza ahadi yake kwa wananchi ya kuongeza pato la Taifa kwa
kukusanya kodi. Azma hii imetekelezwa kwa vitendo kwani mwanzoni mwa
utawala wa Rais Magufuli mapato yatokanayo na kodi yameongezeka kutoka
takriban bilioni mia nane hadi kufikia trilioni 1.3 kwa mwezi.
Hivi karibuni, Rais Magufuli amezindua Mfumo Mpya wa Ukusanyaji kodi kwa njia ya Kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS), mfumo ambao unatarajiwa kuongeza mapato kwa kiwango kikubwa.
Akizindua Mfumo huo, Rais Magufuli
alitoa agizo kwa makampuni ya simu na kusema, “Nimepata taarifa kuwa
hadi sasa Kampuni za simu za TTCL, Hallotel na Smart ndizo pekee
zilizojisajili katika mfumo huu, sasa natoa wito kwa makampuni mengine
na mabenki yahakikishe yanasajisajili kabla ya mwezi Desemba mwaka huu”.
Ili kuwezesha mfumo huo kufanya
kazi, makampuni yote ya simu, mabenki na yale yanayofanya miamala kwa
njia ya kielektroniki yanapaswa kujisajili katika Kituo cha Taifa cha
Kuhifadhia Taarifa (Data Centre) ambacho kina uwezo wakuona kila muamala unaofanyika na kufanya ukokotozi wa kodi inayostahili kulipwa.
Mfumo huu kwa mujibu wa Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, ni sehemu ya
mchakato wa ukusanyaji wa mapato unaojumuisha mifumo mbalimbali
iliyowekwa pamoja kuweza kufanya ukadiriaji, tathmini na ukokotozi wa
kodi kutoka kwenye miamala mbalimbali inayofanyika kielektroniki.
Ni Mfumo ambao unahusisha moduli
tisa zinazofanyakazi mwanzo hadi mwisho kuhakikisha kodi inakusanywa,
inakadiriwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka ya
Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar ambazo zipo Benki Kuu.
Amezitaja moduli hizo kuwa ni : moduli ya kukusanya taarifa, kutunza
taarifa, kuhakiki taarifa na kushirikisha mifumo. Moduli nyingine ni ya
kuzuia udanganyifu, ya kukusanya kodi, ya kutoa ripoti, ya usalama wa
miundombinu na moduli ya kutoa taarifa kwa kinachotokea.
Bwana Kichere anaeleza kuwa
imekuwepo mifumo mingine ya kukusanya mapato kielektroniki ambayo
imeonyesha kuwa na mianya ya kukwepa kodi. Kuhusu mifumo mingine
Kamishna Mkuu anasema baadhi ya mifumo ambayo imeanzishwa na
inatekelezwa kuanzia kipindi cha mwaka 2012 ni kama ifuatavyo:
Electronic Cargo Tracking System (ECTS).
Mwaka 2012 Mamlaka ya Mapato Tanzania iliunda mfumo kufuatilia mizigo
ipitayo katika bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi jirani. Mfumo huu
umesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tatizo la ukwepaji wa kodi kwa
mizigo iliyokusudiwa kupelekwa nchi jirani
Mfumo wa Kielektroniki wa ulipaji
Kodi (Revenue Gateway System) ulianzishwa mwaka 2013 na unawasiliana na
Benki Kuu pamoja na benki za kibiashara hivyo unamuwezesha mlipakodi
kufanya malipo ya kodi mbalimbali kupitia benki au kwa kutumia simu ya
kiganjani akiwa mahali popote na hivyo kuondoa usumbufu kwa mlipakodi.
Pia mfumo huu unawezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za mapato ya
Serikali kwa wakati.
Mfumo wa kielektroniki wa Forodha
yaani Tanzania Customs Integrated System (TANCIS). Mfumo huu ulianzishwa
mwaka 2014 na unatumika kuthaminisha mizigo na kukadiria kodi ili kodi
sitahiki ilipwe pamoja na kuratibu shughuli za uondoshwaji mizigo maeneo
ya forodha. Mifumo hii yote imewezesha kuongeza mapato kutoka wastani
wa shilingi trilioni 3.4 mwaka 2013/14 hadi trilioni 5.2 kwa mwaka
2015/16.
Bwana Kichere anafafanua kuwa
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato
Zanzibar (ZRB) imegundua kwamba kuna mianya ya kimfumo inayoikosesha
serikali mapato kutoka kwa walipakodi mbalimbali.
Changamoto ni kubwa zaidi kwenye
huduma zitolewazo kwa mifumo ya kielektoniki ya makampuni ya simu
(Mobile Network Operators) ambapo wahusika hutoa huduma na kupata mapato
yao mara moja, wakati ambapo kodi (kodi yaongezeko la thamani – VAT na
ushuru wa bidhaa – (Excise Duty) inayopaswa kulipwa kwa serikali
inategemea mawasilisho ya makadirio kutoka kwa makampuni husika. Hali
hiyo, husababisha baadhi ya makampuni kutumia mwanya huo kuipunja
serikali kodi stahiki.
Ili kukabiliana na changamoto
hizi, TRA na ZRB kwa kushirikiana na taasisi nyingine za serikali
zimeunda mfumo utakaowezesha kutathmini, kukusanya na kuhasibu kodi kwa
njia ya kielektoniki moja kwa moja bila kuathiriwa na utashi wa mtu
(without human intervention).
Ndoto ya Rais Magufuli ya kubuni
vyanzo vingine vya ukusanyaji mapato inaanza kutimia baada ya bajeti kuu
ya Serikali kwa mwaka 2017/18 kuanisha vyanzo hivyo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango akiwasilisha makadrio ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa
Fedha unaoanza Julai 1, 2017 anasema, “Serikali itatoza Kodi ya Majengo
kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na
Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango
maalum (flat rate) cha shilingi elfu kumi (10,000) kwa nyumba na
shilingi elfu hamsini (50,000) kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.
“Serikali itawatambua rasmi
wafanyabiashara wadogo wadogo wasio rasmi na wanaofanyia biashara katika
maeneo yasiyo rasmi mfano mama lishe, wauzaji mitumba wadogo, wauza
mazao ya kilimo wadogo kama mboga mboga, ndizi, matunda, na kadhalika
kwa kuwapatia vitambulisho maalum vya kazi wanazozifanya”, alisema Dkt.
Mpango.
Katika kutekeleza suala la
ukusanyaji wa mapato kielektroniki, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi imezindua Mfumo wa kukusanya kodi ya pango la ardhi kwa njia
ya kielektroniki. Mfumo huu umeonyesha kuwa ni bora katika kuongeza
ukusanyaji wa mapato.
Kwa Mfumo huo, mlipaji kodi
hahitaji kwenda Wizarani au kituo cha malipo kulipa kodi bali anaweza
kufanya hivyo akiwa mahali popote kwa kutumia simu yake ya mkononi kwa
kupitia menyu kuu ya Taifa ambayo ni *152*00#. Njia hii itamwondelea
mlipaji usumbufu ikiwemo kupoteza muda mwingi kutoka napokaa na kufika
Wizarani kwa ajili ya kulipia kodi.
Mkuu wa Kitengo cha Kodi wa Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami ansema kuwa
katika kipindi kifupi tangu mfumo huo uanze kutumika, mapato
yameongezeka kwa shilingi milioni 9 ndani ya siku tano. Hii ni kutoka
bilioni 2 hadi bilioni 2.9 kwa siku tano. Mwenendo huu wa ongezeko
unaonyesha kuwa kwa mwezi hadi kwa mwaka mapato yataongezeka kwa kiwango
kikubwa.
Naye Mkurugenzi wa Mifumo ya
Kifedha wa Wizara ya Fedha na Mipango anasema kuwa kwa kutumia mfumo huo
mtu atatumiwa ujumbe wa majibu kuonyesha kiasi cha fedha alicholipia
ambao utahesabika kama risti.
Hakika mifumo hii ikisimamiwa
barabara, ni dhahiri kuwa changamoto za kibajeti zitapungua. Kulipa kodi
ni suala la msingi na ndiyo maana kwenye nukuu za Baba wa Taifa, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuhusu kodi zinasema, “Serikali ya
wala rushwa haiwezi kukusanya kodi”. Mwalimu alisisitiza ukusanyaji wa
kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi zikiwemo huduma za kijamii kama
vile; elimu, afya, maji safi na salama na miundombinu.
Tags
KODI