Msajili wa Baraza la Famasi
Tanzania Bi. Elizabeth Shekalaghe akisisitiza jambo wakati akifungua
mafunzo ya siku moja kwa wafamasia wanaotarajiwa kuanza kutoa huduma
mara baada ya kuhitimu masomo yao na kula kiapo cha kuzingatia maadili
ya taaluma hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Naibu Msajili wa Baraza hilo Bi.
Zainabu Nyamungumi akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja kwa
wafamasia wanaotarajiwa kuanza kutoa huduma baada ya kuhitimu masomo yao
na kula kiapo,Leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Usajili wa Baraza hilo Bw.Rashid Kiria akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo hayo.
Mmoja wa wafamasia hao akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika mapema leo Jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………………..
Frank Mvungi-Maelezo
Wafamasia nchini wametakiwa
kuzingatia maadili na weledi katika kutekeleza majukumu yao ili
kuchochea azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kutoa huduma bora za afya
kote nchini hali itakayochea maendeleo na ukuaji wa sekta hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Msajili wa Baraza la Famasi nchini Bi. Elizabeth Shekalaghe
wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa wafamasia waliohitimu masomo
yao hivi karibuni katika vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi na
kula kiapo cha kuzingatia maadili ya taaluma hiyo adhimu kwa mustakabali
wa ukuaji wa sekta ya afya hapa nchini.
“Mafunzo haya yamehusisha
takribani wafamasia 160 na yanalenga kuwakumbusha wajibu wao na umuhimu
wa kuzingatia maadili na kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza
wakati watakapokuwa wanatekeza majukumu yao kwa kuwa wapo watakafanya
kazi katika Mikoa, Halmashauri na Hospitali katika maeneo mbalimbali “
alisisitiza Shekalaghe.
Akifafanua amesema kuwa mafunzo
hayo yameshafanyika katika Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini,Kaskazini,Mashariki na Kanda ya Ziwa dhamira ikiwa kuwajengea
uwezo wafamasia wanaohitimu kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yao mara
baada ya kula kiapo.
Aliongeza kuwa jukumu la Baraza
hilo ni kufuatilia mwenendo wa wafamasia ili kuhakikisha kuwa
wanazingatia maadili ya taaluma hiyo na wamiliki wa maduka ya dawa
kuhakikisha kuwa wanaajiri wafamasia wenye sifa na waliosajiliwa ili
watoe huduma bora kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Kwa upande wake Naibu Msajili wa
Baraza hilo Bi. Zainabu Nyamungumi akiwasilisha mada katika mafunzo hayo
amesisitiza umuhimu wa wafamasia kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na
taratibu zinazosimamia taaluma hiyo katika maeneo watakayokuwa wanafanya
kazi.
Pia aliwataka kutekeleza kwa vitendo yale waliyofundishwa katika mafunzo hayo ili kuchochea ukuaji wa taaluma hiyo.
Naye mdau wa Taaluma hiyo ambaye
pia ni mwanataaluma Bw. Manase Kejo iliwataka wafamasia hao kujiamini na
kujiajiri kwa kuwa taaluma waliyo nayo ni fursa inayoweza kuzalisha
ajira.
“Ni muhimu mkatambua kuwa taaluma hii ni muhimu na jambo kubwa ni kutambua kuwa mnaweza kujiajiri,” Alisisitiza Kejo.
Mwaka 2013 Tanzania ilikuwa na
wafamasia takribani 450 na kufikia mwaka 2017 wamefikia 1600 hali
inayoonyesha kuwa taaluma hiyo inaendelea kukua kwa kasi suala
linalochagizwa na ongezeko la vyuo vinavyotoa taaluma hiyo kikiwemo
Chuo Kikuu cha Mtakatifu John Dodoma, Bugando na Chuo Kikuu cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili.
Tags
MASAI