Mkuu wa Kitengo cha Tehama na
Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3)
bwana Desderi Wengaa akizungumza na waratibu elimu kata na waganga
wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na
Mtwara DC (hawapo pichani) kuhusu malengo ya kuanzishwa kwa mfumo mpya
wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama
Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Baadhi ya Waganga wafawidhi wa
vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC
wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi
Sambwe Sijabaje (hayupo pichani) wakati alipofungua mafunzo ya siku
mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa
za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting
and Reporting System (FFARS).
Baadhi ya Waratibu wa Elimu Kata
kutoka Manispaa ya Mtwara Mikindani na Mtwara DC wakimsikiliza Kaimu
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje
(hayupo pichani) wakati alipofungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna
ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha
unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and
Reporting System (FFARS).
Sehemu ya Waratibu wa Elimu Kata
na Waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Mtwara
Mikindani na Mtwara DC wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya
Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (hayupo pichani) wakati
alipofungua mafunzo ya siku mbili kuhusu namna ya kuutumia mfumo mpya wa
uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa Kiingereza kama
Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya
Mtwara Mikindani Mhandisi Sambwe Sijabaje (aliyeketi katikati) akiwa
pamoja na baadhi ya waratibu wa elimu kata kutoka Halmashauri ya Wilaya
ya Mtwara mara baada ya ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kuhusu namna
ya kuutumia mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha
unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and
Reporting System (FFARS). Aliyeketi kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Tehama
na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma
(PS3) bwana Desderi Wengaa
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Waganga wafawidhi wa vituo vya
afya, na Waratibu elimu kata kutoka Halmashauri 93 zilizo katika mikoa
13 nchini inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma
(PS3) nchini wameanza mafunzo ya siku mbili juu ya namna ya kutumia
mfumo mpya wa uhasibu na utoaji taarifa za fedha unaojulikana kwa
Kiingereza kama Facility Financial Accounting and Reporting System (FFARS).
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo
cha Tehama na Mawasiliano kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta
za Umma (PS3) bwana Desderi Wengaa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea
uwezo watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma na kusaidia
upatikanaji wa taarifa sahihi katika mahesabu ya mapato na matumizi ya
halmashauri.
Bwana Wengaa alisema kuwa
kuunda kwa mfumo huo kutasaidia kuhakikisha fedha za ruzuku zinasimamiwa
vizuri na taarifa za matumizi yake zinatolewa kwa usahihi tofauti na
ilivyokuwa mwanzo.
Alisema kuwa FFARS itawapatia
watoa huduma mfumo sanifu uliorahisishwa ambao utawawezesha kutunza
taarifa za fedha zinazotolewa na zilizopo katika vituo vyao.
Bwana Wengaa aliongeza kuwa
FFARS itaweza kufuatilia matumizi ya fedha hizo katika kufikia malengo
ya utoaji huduma na kuhakikisha yanaendana na sheria za manunuzi na
utoaji taarifa.
“Taarifa hizi zitasaidia
Serikali kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Umma na kuongeza
uwazi, na hivyo watoa huduma wa afya kuwa na wajibu kwa jamii
wanayoihudumia,” alisema.
Alisema kuwa mafunzo hayo
yanafanyika katika Mikoa 13 ya Tanzania Bara inayotekeleza Mradi wa
Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ambapo waratibu elimu kata
na waganga wafawidhi wa vituo vya afya wanashiriki.
Aliitaja mikoa hiyo 13 kuwa
ni pamoja na Mtwara, Lindi, Dodoma, Iringa, Mbeya, Njombe na Morogoro.
Mikoa mingine ni Mara, Mwanza, Rukwa, Shinyanga, Kigoma, na Kagera.
Mafunzo hayo yanafanyika
katika ngazi ya halmashauri, ambapo mjini Mtwara mafunzo hayo
yaliwahusisha waganga wafawidhi wa vituo vya afya, na Waratibu elimu
kata kutoka Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani na Halmashauri
ya Wilaya ya Mtwara.
Akifungua mafunzo hayo kwa
niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bibi Beatrice
Dominick, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mhandisi Sambwe Sijabaje
alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watoa huduma wa vituo vya
halmashauri hizo mbili kuwa na mfumo maalum wa kuandaa taarifa za mapato
na matumizi, na hivyo kuchangia uwajibikaji na utoaji wa huduma bora
kwa wananchi.
Alisema kuwa mafunzo hayo
yanatolewa kwa mfumo wa kielektroniki ili kuendana na wakati na
mabadiliko ya teknolojia na mfumo wwa kujaza vitabu ulioboreshwa ili
kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo umeme na kukosekana
kwa huduma ya mtandao wa intaneti kwa baadhi ya vituo vya kutolea
huduma.
Hata hivyo baadhi ya washiriki
wa mafunzo hayo kutoka Halmashauri za Manispaa ya Mtwara Mikindani na
Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wameiomba Serikali kuwapatia vitendea
kazi kama vile Laptop ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi
uliokusudiwa.
Mfumo huo wa FFARS
unatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID.
Mafunzo hayo yanatarajiwa
kuwanufaisha Waganga wafawidhi wa vituo vya afya, na Waratibu elimu kata
kutoka zaidi ya Vituo vya Afya 550, Zahanati 6800, Hospitali za Wilaya
135, na takribani Shule za Msingi na Sekondari 20,000 katika mikoa yote
26 ya Tanzania Bara.
Tags
ELIMU