Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwapungia wananchi wakati alipokagua eneo la ujenzi wa jengo la pamoja
la forodha kwenye mpaka wa Tanzania na Zambia katika mji mdogo wa
Tunduma. Alikuwa katika ziara ya mkoa wa Songwe Julai 21, 2017. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba
kuanzisha mradi wa ujenzi wa hospitali.
Amesema Sh. milioni 900
zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Halmashauri kwa sasa zianze
kutumika katika kuanzisha ujenzi wa hospitali hiyo.
Agizo hilo alilitoa jana jioni
(Ijumaa, Julai 21, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano
wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Tunduma.
“Kwa kuwa afya ni jambo muhimu
katika utekelezaji wa kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya Hapa Kazi
Tu, hivyo naagiza fedha zilizotengwa kuanza ujenzi wa ofisi zitumike
katika ujenzi wa hospitali.”
Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa
halmashauri hiyo kuongezea sh. milioni 126 katika ujenzi huo. Fedha
hizo zilitengwa kwa ajili ya kuwafidia wamiliki wa eneo lililotengwa
awali kwa ajili ya kujenga hospitali, ambapo aliwataka watafute eneo
lisilohitaji fidia.
Pia, Waziri Mkuu aliuagiza
uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) iandae ramani kwa ajili ya
ujenzi wa hospitali hiyo na kuhusu suala la ujenzi wa ofisi Serikali
italishughulikia.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo
baada ya Mbunge wa jimbo la Tunduma, Mheshimiwa Frank Mwakajoka
aliyeiomba kuiomba Serikali kuwajengea hospitali kwa kuwa halmashauri
hiyo haina hospitali, hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi
pale wanapohitaji huduma hiyo.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo, Bw.
Juma Irando alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili wilaya hiyo kuwa
ni ukosefu wa hospitali ya wilaya, ukosefu wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya na
ofisi za Halmashauri.
Pia changamoto nyingine ni ubovu
wa miundombinu ya barabara iliwemo ya Makamba-Ikana inayotakiwa
kukarabatiwa inayounganisha ukanda wa juu na chini ili wananchi wa
ukanda wa juu waweze kufika makao makuu ya wilaya.
Tags
AFYA